Friday 13 February 2009

Scolari: 'Timu ilikosa 'Mchawi', walizoea soka la 'Umangimeza!''

Luiz Felipe Scolari, alietimuliwa kazi na Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich siku ya Jumatatu, alitoboa siri ya kudebweda Chelsea alipofanya mahojiano na Gazeti la Ufaransa 'France Football' wiki iliyokwisha wakati hajui hatima yake nini!
Scolari alikiri Chelsea haina ubunifu na Wachezaji kama Florent Malouda, Didier Drogba na Salomon Kalou viwango vyao vimeshuka sana na vinatisha.

Scolari alitamka: 'Hapa Chelsea hatuna Mchezaji mbunifu anaeweza kuleta 'uchawi' na kuibadilisha mechi sekunde moja! Zamani alikuwepo Arjen Robben na aliweza kubadilisha mechi kwa uwezo wake binafsi! Robinho angekuwa hapa angeweza kufanya hivyo, haogopi kupiga chenga na hushambulia bila woga. Mimi kama Mbrazil napenda hilo! Timu yangu si ya Kibrazil! Ni timu inayocheza soka la 'Umangimeza' haina Wachezaji wabunifu! Ndio maana naamini Robinho angefanya mengi kwa timu hii!'
Alipoulizwa kwa nini hakuwa anawechezesha Didier Drogba na Nicolas Anelka kama Washambuliaji wawili kwenye Fomesheni ya 4-4-2, Scolari alijibu: 'Sina Wachezaji wanaoweza kubadilika kumudu mfumo huo. Ilikuwa ngumu wao kucheza pamoja. Sina Wachezaji wa kucheza Wingi. Kalou anaweza kucheza kwenye 4-3-3 lakini 4-4-2 hawezi, ingawa anaweza kucheza Winga kulia kwa sababu tukishambuliwa hana uwezo mzuri kurudi nyuma kusaidia ulinzi! Na nani atacheza Winga ya kushoto?'
Scolari aliendelea: 'Hata tukicheza 4-4-2 nani viungo? Tutazidiwa kwenye midifildi! Inabidi nichague mmoja acheze Drogba au Anelka. Lakini Drogba baada ya kuumia hayupo kwenye fomu, anakosa kujiamini. Malouda wa Chelsea si Malouda wa Lyon'
Scolari alimaliza mahojiano hayo na Gazeti 'France Football' kwa pengine, bila kujijua, kutoa utabiri wake: 'Chelsea ndio walinipa kazi mwanzoni mwa msimu uliokwisha. Huo ulikuwa uamuzi wao. Sasa, wakitaka kunifukuza, huo uamuzi wao. Mimi nafanya kazi yangu tu!'

No comments:

Powered By Blogger