Tuesday 15 September 2009

Besiktas v Manchester United
Manchester United, leo ugenini ndani ya Inonu Stadium huko Uturuki, itavaana na Besiktas ikiwa ni siku 111 tangu wafungwe 2-0 Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na FC Barcelona huko Rome.
Man U, wakiongozwa na Meneja wao Sir Alex Ferguson pamoja na Wachezaji wao Maveterani, wamekiri kipigo cha Rome kimewakera sana na sasa wanaomba wakutane tena na Barcelona ili walipe kisasi.
Man United wanasafiri kwenda Uturuki mara baada ya ushindi mtamu wa ugenini kwenye LIGI KUU England walioupata baada ya kuichabanga Tottenham mabao 3-1 huku wakitandaza ‘Soka Tamu!’
Man United wako Kundi moja na Besiktas, CSKA Moscow na VfB Wolfsburg.
Besiktas, wakiongozwa na Kocha Mustafa Denizli, wataingia uwanjani leo mara tu baada ya kupigwa mabao 3-0 na Mahasimu wao wa Mjini Instanbul Timu ya Galatasaray siku ya Jumamosi.
Huko Uturuki, Timu zinazonguruma sana ni Fenerbahce na Galatasaray lakini msimu huu ni Besiktas pekee ndio wamo UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Mechi ya leo itamkutanisha Kipa wa zamani wa Uturuki, Rustu Recber, na Wayne Rooney kwa mara ya kwanza tangu Rooney amtoboe Recber kwa bao 3 mguuni kwake kwenye mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE iliyochezwa Old Trafford mwaka 2004 kati ya Man United na Fenerbahce na Rustu Recber akiwa Kipa wa Fenerbahce na Rooney akiichezea Man U mechi yake ya kwanza tangu anunuliwe toka Everton. Man U walishinda mechi hiyo 6-2.
Waamuzi wa mechi hii ni kutoka Italia watakaoongozwa na Refa Nicola Rizzoli.
Chelsea v FC Porto
Chelsea wanaanza kampeni ya kutwaa Kombe la UEFA CHAMPIONS LEAGUE, ambalo hawajawahi kulitwaa, wakiwa nyumbani Stamford Bridge kwa kucheza na FC Porto ya Ureno.
Chelsea, katika misimu miwili iliyopita, walikaribia mno kutwaa Kombe hilo lakini kwa mara zote walibwagwa kwa uchungu.
Msimu wa 2007/8 walifika Fainali na kutolewa na Manchester United kwa penalti na hivyo kulikosa Kombe.
Msimu uliopita, baada ya kutoka suluhu 0-0 ugenini na Barcelona katika Nusu Fainali, walibwagwa kwao Stamford Bridge wakiwa wanaongoza 1-0 hadi dakika za majeruhi ndipo Andres Iniesta wa Barcelona akasawazisha bao na kuwaingiza Barcelona Fainali kwa goli la ugenini.
Uchungu na hasira ya kubwagwa mechi hiyo iliwasababisha Wachezaji wa Chelsea, Didier Drogba na Jose Bosingwa, wapandwe jazba na kumzonga, kumtukana na kumkashifu Refa.
UEFA iliwafungia Drogba na Bosingwa kwa vitendo hivyo na wataikosa mechi ya leo.
Kwa sasa Chelsea wanae Meneja mpya msimu huu, Mtaliana Carlo Ancelotti, ambae ameshawahi kuuchukua Ubingwa wa Ulaya akiwa na Klabu ya AC Milan.
Msimu huu, Chelsea wamecheza mechi 5 za LIGI KUU na kushinda zote.
FC Porto, chini ya Meneja Jesualdo Ferreira, msimu uliokwisha kwenye Kombe hili walitolewa Robo Fainali na Manchester United kwa jumla ya mabao 3-2.
Msimu huu, FC Porto, huko kwao, wameshacheza mechi za Ligi 4 na kutofungwa mpaka sasa.
Waamuzi wa mechi ya leo wanatoka Austria na Refa ni Konrad Plautz.

No comments:

Powered By Blogger