Yanga, Simba zafukuzana Ligi Kuu Vodacom
Yanga ipo kileleni na Simba wako nyuma yao kwa pointi moja baada ya mechi 6 za Ligi Kuu Vodacom.
Wakongwe hao wataumana huko CCM Kirumba Mwanza Oktoba 16 huo ukiwa Uwanja wa nyumbani wa Simba.
Uwanja wa Jamhuri huko Morogoro ndio 'homu graundi' ya Yanga baada ya Timu hizo mbili kutimuliwa Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam ambao uko matengenezoni.
Mpaka sasa Yanga wana pointi 16 baada ya kushinda mechi 5 na sare moja huku Simba wana pointi 15 kwa kushinda mechi 5 na kufungwa moja.
FIFA yaifungia Nigeria
FIFA imeifungia Nigeria kutocheza mashindano yeyote ya Kimataifa baada ya Chama cha Soka cha Nigeria, NFF, kuingiliwa katika uendeshwaji wake na Serikali.
Hatua ya FIFA imefuatia kuburutwa Mahakamani Viongozi kadhaa wa NFF na Kikundi kimoja kinachodai uchaguzi wa Viongozi wa NFF haukuwa halali.
Vilevile, Kamisheni ya Michezo ya Nchi hiyo ilitaka kulazimisha Ligi ya huko ianze Msimu mpya bila ya Timu yeyote kuteremshwa Daraja.
Hatua hizo zimeifanya FIFA itoe amri ya kuisimamisha Nchi hiyo na hivyo kuleta kizaazaa juu ya hatma ya mechi ya Wikiendi hii ya Makundi ya Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Guinea na Nigeria huko Conakry, Guinea.
No comments:
Post a Comment