Man United waifumua Man City na kutinga Fainali!!!!
• Ni Rooney aleta ushindi!!!!
Huku ngoma ikiwa suluhu kwa jumla ya magoli 3-3, Wayne Rooney alichomeka bao la ushindi dakika za majeruhi na kuwanyamazisha mahasimu wao wakubwa Manchester City na pia kuipeleka Manchester United Fainali ya Kombe la Carling huko Wembley hapo Febryari 28 watakapocheza na Aston Villa.
Bao la Wayne Rooney liliipa ushindi Man U wa bao 3-1 hapo jana kwao Old Trafford.
Man City walishinda mechi ya kwanza 2-1 na hivyo wametolewa kwa jumla ya bao 4-3.
Man City waliingia kwenye mechi hiyo wakiwa mbele kwa bao 2-1 na majigambo yao, wakiongozwa na kidomodomo cha Tevez, lakini walisahau kuwa wao kwa mara ya mwisho kutinga Fainali yeyote ilikuwa ni mwaka 1981 na tangu wakati huo mpaka sasa Manchester United wameshacheza Fainali 21 na kutwaa Ubingwa wa England mara 11.
Hadi mapumziko bao zilikuwa 0-0.
Paul Scholes alifunga bao la kwanza dakika ya 51 na Michael Carrick akapachika la pili dakika ya 71 lakini Tevez akawapa City matumaini alipofunga bao dakika ya 75.
Huku ngoma ikitaka kwenda dakika 30 za nyongeza ndipo Rooney akaonyesha ushujaa wake kwa mara nyingine tena.
MATOKEO MECHI ZA Jumatano, Januari 27
Caling Cup
Man United 3 v Man City 1 [Man U aingia Fainali kwa jumla ya bao 4-3]
LIGI KUU
Aston Villa 0 v Arsenal 0
Chelsea 3 v Birmingham 0
Blackburn 2 v Wigan 1
Everton 2 v Sunderland 0
Basturk asaini Blackburn
Mchezaji wa Kimataifa wa Uturuki, Yildiray Basturk, miaka 31, ambae ni Mzaliwa wa Ujerumani amehamia Klabu ya Ligi Kuu England Blackburn Rovers kutoka Klabu ya Bundesliga huko Ujerumani ya Stuttgart.
Basturk, ambae ni Kiungo, ameshaichezea Timu ya Taifa ya Uturuki mara 49 na amesema alidokezwa kuwa Blackburn ni Klabu nzuri na Mchezaji wa zamani wa Blackburn Mturuki Tugay ambae amestaafu.
Basturk amesaini mkataba wa kuichezea Blackburn hadi mwishoni mwa Msimu huu.
Rio akana shitaka la FA
Mchezaji wa Manchester United Rio Ferdinand amekana shitaka lake la kucheza vibaya na kumshambulia Mchezaji wa Hull City Craig Fagan analodaiwa na FA kulitenda kwenye mechi ya Ligi Kuu Jumamosi iliyokwisha ambayo Man United walishinda 4-0.
Refa Steve Bennett hakuona kitendo cha Rio lakini alimpa Fagan Kadi ya Njano mara baada ya Rio kuonekana akitenda kosa hilo.
Kwa kukanusha kosa, Rio yuko huru kucheza mechi ya Nusu Fainali ya Carling dhidi ya Manchester City na jopo litasikiliza kesi yake Alhamisi Januari 28 na endapo atapatikana na hatia atafungiwa mechi 3 na hivyo kuikosa mechi ya Jumapili na Arsenal, mechi ya Februari 6 na Portsmouth na ile dhidi ya Aston Villa siku 4 baadae.
No comments:
Post a Comment