Saturday, 23 May 2009

CHELSEA YATOA TAMKO KUHUSU MASHTAKA YA UEFA!!
===YASIKITISHWA KUSHTAKIWA!!!
===MENEJA WAO HIDDINK ADAI UEFA IMENUFAIKA KWA FAINALI KUTOKUWA YA TIMU MBILI ZA ENGLAND!!
Klabu ya Chelsea imetoa tamko rasmi kufuatia hatua ya UEFA, Chama cha Soka Ulaya, kuwashitaki kama Klabu kwa kushindwa kudhibiti Wachezaji wake wasifanye utovu wa nidhamu na pia kushindwa kuwazuia Washabiki wake wasitupe vitu uwanjani huku Wachezaji wake Didier Drogba na Jose Bosingwa wakiwemo kwenye mashtaka kwa kutuhumiwa kumkashifu Refa Tom Henning Ovrebo kutoka Norway aliechezesha pambano lao la Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE dhidi ya Barcelona lililoisha 1-1 lakini Chelsea wakatupwa nje kwa goli la ugenini.
Taarifa ya Chelsea ilisema: ‘Chelsea itajibu tuhuma za UEFA leo kwa niaba ya Klabu na Wachezaji waliotuhumiwa. Tunapenda kuweka wazi, kama tulivyofanya wakati ule, matukio yale yanasikitisha na yalitokea tu baada ya kupandwa na munkari kufuatia kushindwa katika mazingara yenye utata katika mechi muhimu.’
Taarifa hiyo ilimaliza kwa kukumbusha kuwa Wachezaji wake Drogba na Bosingwa walishaomba msamaha kwa vitendo vyao.
Chelsea na Wachezaji wao wamepewa mpaka Ijumaa ijayo Mei 29 kutoa utetezi na UEFA itakaa Juni 17 kusikiliza kesi hiyo.
Wakati huohuo, Meneja wa Chelsea, Guus Hiddink, amekoleza moto katika sakata hilo la kushindwa Chelsea kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE na Barcelona na sasa kuzikutanisha Fainali Manchester United na Barcelona hapo Jumatano huko Roma, Italia.
Guus Hiddink amedai UEAFA inapata manufaa makubwa kwa Barcelona kucheza na Manchester United Fainali badala ya Timu mbili za England kukutana tena Fainali kama ilivyokuwa msimu uliopita huko Moscow, Urusi Chelsea walipotolewa na Manchester United.
Hiddink anasema: ‘Ni ngumu kusema kama kulikuwa na njama kwa sababu hatuna ushahidi!! Lakini mimi ni binadamu na nadhani UEFA, ingawa hawawezi kusema hilo, wana furaha kubwa hamna Fainali ya Timu za England tupu kwa mara ya pili!! Lakini kosa ni letu!! Tungefunga goli nyingi mechi ile!! Ila Refa Yule ni mzoefu ingawa ashawahi kuwa na matatizo hapo nyuma! Sijui nini kilimtokea usiku ule!!
Katika mechi hiyo kitu kilichowakera Chelsea ni kunyimwa penalti kadhaa za wazi.
RAFA: ‘ALONSO HAUZWI!!’
Meneja wa Liverpool, Rafa Benitez, ameibuka na kung’ang;ania Kiungo wake Xabi Alonso atabaki Anfield baada ya Magazeti kadhaa huko England na Spain kubeba mabango kuwa Kiungo huyo yuko njiani kuelekea Real Madrid kufuatia kauli za Mgombea Urais wa Real Madrid Florentino Perez kudai atamsaini.
Msimu uliopita Xavi Alonso alikuwa bado kidogo auzwe kwani Liverpool ilionyesha nia ya wazi kabisa kutaka kumchukua Nahodha wa Aston Villa Greth Barry dili ambayo baadae ilikwama baada ya mvutano wa bei kati ya Klabu hizo mbili. Wakati huo, Xavi Alonso alikuwa majeruhi lakini alipopona, msimu huu, Alonso ameng’ara sana kwenye mechi alizochezea Liverpool.
Benitez amesema: ‘Xavi bado ana miaka mitatu kwenye mkataba wake na hatutaki kumuuza.’
UTATA KIKOSI CHA MAN U KITAKACHOPANGWA MECHI YA KESHO NA HULL CITY!!!!
===Ferguson alifikiria awapigie simu Mameneja wa Sunderland, Newcastle na Middlesbrough ili kuwapoza!!!!!
Bosi wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amewahakikishia Mameneja wa Klabu za Sunderland, Newcastle na Middlesbrough kwamba siku ya Jumapili watakapocheza mechi ya mwisho ya LIGI KUU England huko KC Stadium na wenyeji Hull City atapanga Kikosi imara chenye uwezo wa kushinda mechi hiyo.
Huko England, huku Manchester United tayari keshaunasa Ubingwa wa LIGI KUU na Jumatano ana ‘BIGI MECHI’ na Barcelona ikiwa Fainali ya Ubingwa wa Ulaya, kumekuwa na mjadala mkali kuhusu Kikosi kitakachopangwa na Ferguson kwenye mechi hiyo na Hull City ambayo inapigania kufa na kupona ishinde ili inusurike kushushwa Daraja wakati Timu za Sunderland, Newcastle na Middlesbrough zinaomba Hull City afungwe ili na wao wapone kushushwa Daraja.
Ili kupoza mjadala huo na kuwaondolea wasiwasi wahusika, Ferguson amesema: ‘Kitu muhimu tuwe na Ligi yenye uaminifu na uadilifu mkubwa duniani na sisi tutatimiza wajibu wetu Jumapili! Timu yeyote itayoshuka uwanjani itaiwakilisha Manchester United na kama kawaida sisi tutacheza tushinde tu! Mtu yeyote asiwe na wasiwasi kuhusu dhamira yetu safari hii!’
Ferguson akaongezea: ‘Nilifikiria niwapigie simu Mameneja watatu wahusika-Gareth Southgate [Middlesbrough], Ricky Sbragia [Sunderland] na Alan Shearer [Newcastle]. Lakini nikafikiria Ricky Sbragia alifanya kazi hapa Man U na anaijua Klabu hii na lazima atajua nini tutafanya! Southgate na Shearer mara nyingi sana washacheza na sisi na wanajua wazi Man U ikicheza inatafuta nini!!’
Lakini, Ferguson akakubali anaweza kupeleka Kikosi cha Wachezaji Chipukizi kama kile kilichocheza Wembley kwenye Nusu Fainali ya FA CUP na kutolewa kwa matuta na Everton ambacho baadhi ya Wachezaji wake walikuwa Darron Gibson, Federico Macheda na Danny Welbeck.
Ferguson akaongeza: ‘Ikiwa niliwaamini kucheza Nusu Fainali ya Kombe muhimu, kwa nini nisiwaamini kucheza mechi ya mwisho ya Ligi wakati tushachukua Ubingwa?’
Hata hivyo, Ferguson akamalizia kwa kuiponda FA: ‘Barcelona wamecheza mechi yao ya mwisho ya Ligi Jumamosi na sisi Jumapili! Timu ya England imeingia Fainali sasa mara ya 5 mfululizo, sidhani FA hawajui hilo! Ni rahisi kwao kuzipanga hizi mechi za mwisho za Ligi ziwe Jumamosi badala ya Jumapili. Hata ingekuwa Jumamosi, nisingepanga Kikosi changu chote bora ila labda Wachezaji wawili au watatu wangekuwemo!’

No comments:

Powered By Blogger