Thursday 21 May 2009

Bosi wa Arsenal Gazidis athibitisha Wenger kubaki Arsenal!!!
Mkurugenzi Mtendaji wa Arsenal, Ivan Gazidis, amesisitiza Meneja wao Arsene Wenger lazima atabaki Emirates Stadium na kauli hii inafuatia ile ya Wenger mwenyewe hapo jana alipotamka hamna ishu ya yeye kuondoka.
Wenger amekuwa akihusishwa kuhamia Real Madrid baada ya misimu minne kupita huku Arsenal ikiambulia patupu na kutoka bila Kombe lolote. Hali hii imezua manung’uniko toka kwa Wadau na Washabiki wa Klabu.
Gazidis amethibitisha Wenger atabakia na mkataba wake utakapoisha 2011 ataongezewa.
Bosi wa LIGI KUU atetea Klabu kubadilisha Vikosi vyao!!!
Bosi wa LIGI KUU England, Richard Scudamore, amesisitiza Timu ya Manchester United ikiongozwa naSir Alex Ferguson wana kila haki ya kukishusha uwanjani Kikosi chenye Wachezaji wowote wale waliosajiliwa katika mechi yao ya mwisho ya LIGI KUU wakatakapoumana na Hull City Jumapili ijayo.
Wakati mechi hii haina umuhimu wowote kwa Manchester United kwani washatwaa Ubingwa wa LIGI KUU, kwa Hull City mechi hii ni ya kufa na kupona ili kujinusuru kushushwa Daraja.
Timu nyingne ambazo zinaitolea macho mechi hii ni Newcastle na Middlesbrough ambao wanaomba Hull City afungwe ili nao wanusurike kushushwa Daraja.
Manchester United wiki ijayo Jumatano huko Roma, Italia watavaana na Barcelona kwenye Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ambayo Man U wanataka kuwa Timu ya kwanza kabisa kutetea vyema taji lake kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE. Hivyo, Wadau wengi wanaona ni busara kubwa kwa Manchester United kuwapumzisha Mastaa kama Ronaldo, Rooney, Vidic, Van Der Sar na kadhalika katika mechi ‘uchwara’ ya LIGI KUU ya Jumapili ambao wao tayari wameshautwaa Ubingwa.
Richard Scudamore, Mkurugenzi Mtendaji wa LIGI KUU, anaelezea: ‘Lazima tuwe wakweli! Wao washashinda LIGI KUU na Jumatano wana mechi kubwa na Barcelona! Wana Kikosi kikubwa cha Wachezaji wengi sasa kuna ubaya gani kubadilisha Timu? Wao wakishusha Timu yeyote lazima watakuwa wanaamini itashinda!!’
RIO: 'NTACHEZA FAINALI NA BARCELONA!!!'
Beki mahiri wa Manchester United, Rio Ferdinand, ambae yuko nje ya uwanja kwa karibu mwezi sasa baada ya kuumia kwenye mechi kule Emirates Stadium Manchester United ilipoitoa Arsenal 3-1 kwenye Nusu Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, amesema ana imani kubwa atakuwa fiti kucheza Fainali ya Kombe hilo Jumatano ijayo huko Roma, Italia dhidi ya Mabingwa wa Spain, Barcelona.
Jana, Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, alionyesha wasiwasi kuwa huenda Rio akaikosa Fainali hiyo na kudokeza ikiwa atafanya mazoezi vizuri basi inabidi acheze mechi ya LIGI KUU Jumapili na Hull City ili kujipa mazoezi.
Rio Ferdinad alizungumza: ‘Nipo fiti. Nishaanza mazoezi makali. Na Meneja akinichagua ntacheza Jumapili. Sina wasiwasi niko fiti kucheza Fainali na Barcelona.’

No comments:

Powered By Blogger