Saturday, 8 May 2010

Motta kuikosa Fainali UEFA CHAMPIONS LIGI
• Afungiwa Mechi 2
Bodi ya Nidhamu na Udhibiti ya UEFA imemfungia Mchezaji wa Inter Milan Thiago Motta kwa mechi mbili ikiwa ni adhabu baada ya kupewa Kadi Nyekundu mechi ya Nusu Fainali ya pili Inter waliporudiana na FC Barcelona Uwanjani Nou Camp Aprili 28.
Kifungo hicho kinamaanisha Motta hataruhusiwa kucheza Fainali ya UEFA CHAMPIONS LIGI hapo Mei 22 Inter watakapoikwaa Bayern Munich.
Inter wamepewa siku tatu kukata rufaa lakini kawaida ya UEFA ni kuwa rufaa siku zote hutupiliwa mbali.
Motta anaungana na Mchezaji wa Bayern Munich Franck Ribery kukosa Fainali hiyo kwa kufungiwa na UEFA.
Ribery yamemkuta kama ya Motta alipotolewa kwa Kadi Nyekundu kwenye Nusu Fainali Bayern walipocheza na Lyon na UEFA ikampa adhabu ya kufungiwa mechi zaidi.
Bayern walimkatia rufaa Ribery lakini UEFA ikaitupa rufaa hiyo na sasa Bayern wamekwenda CAS [Court of Arbitration for Sports], Mahakama ya Usuluhisho kwa Michezo ili kumwezesha kucheza Fainali.
Togo huru!!
 -Blatter wa FIFA aokoa jahazi!!
Kufuatia usuluhishi wa Sepp Blatter, Rais wa FIFA, Togo itafutiwa adhabu yake ya kufungiwa na CAF, Shirikisho la Soka Afrika, kucheza Mashindano mawili ya Kombe la Mataifa ya Afrika waliyopewa kwa kujitoa Fainali za mashindano kama hayo yaliyofanyika Nchini Angola mwezi Januari baada ya Basi lao kushambuli kwa risasi na Waasi wa Jimbo la Angola la Cabinda na kumuua Dereva wa Basi hilo pamoja na Maafisa wawili wa Togo.
Blatter ametamka: “Nina furaha kusema tumepata ufumbuzi ulioridhisha pande zote. Mafanikio haya ni kwa Jamii yote ya Soka hasa ya Afrika.”
Rais wa CAF, Issa Hayatou, amekubali kuiomba Kamati Kuu ya CAF kuifuta adhabu kwa Togo ambayo ingewafanya wasicheze Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 na 2014.
Baada ya kufungiwa, Togo walikata rufaa kwa CAS [Court of Arbitration for Sports], Mahakama ya Usuluhisho kwa Michezo, na Mahakama hiyo ikamwomba Sepp Blatter kusuluhisha.
Hatua hii ya kuifungulia Togo itawalazimu CAF kurekebisha Ratiba ya Mtoano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 ambayo ilishapangwa mwezi Februari bila Togo kushirikishwa.
Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika ya mwaka 2012 zitafanyika kwenye Nchi mbili kwa pamoja ambazo ni Gabon na Equatorial Guinea na zile za mwaka 2014 zitakuwa Libya.

No comments:

Powered By Blogger