Saturday 8 May 2010

Redknapp Meneja Bora Ligi Kuu 2009/10
Meneja wa Tottenham Harry Redknapp amenyakua Tuzo ya kuwa Meneja Bora wa Msimu.
Redknapp, miaka 63, amepewa Tuzo kwa kutambua mafanikio yake kwa kuiongoza Tottenham inyakue nafasi ya 4 Ligi Kuu na hivyo kuiwezesha kucheza UEFA CHAMPIONS LIGI Msimu ujao kwa mara ya kwanza katika historia yao.
Mwenyewe Redknapp amesema: “Nimefurahi kuzawadiwa lakini bila ya wenzangu Makocha, kina Kevin Bond, Joe Jordan, Clive Allen, Tony Parks, Tim Sherwood, Les Ferdinand na lile jopo la Wakufunzi wa Stamina na Viungo, nisingepata Tuzo hii!”
Redknapp alichukua hatamu Tottenham Oktoba 2008 huku Timu ikiwa mkiani kwenye Ligi Kuu na Msimu huu ipo nafasi ya 4 na inawezekana hata kuipiku Arsenal na kushika nafasi ya 3 ikiwa wataifunga Burnley na Arsenal kufungwa na Fulham siku ya Jumapili.
Redknapp amekuwa Meneja wa pili kushinda Tuzo hii tangu Ligi Kuu ianzishwe bila Timu yake kuwa Bingwa.
Meneja wa kwanza kuikwapua Tuzo bila ya kuwa Bingwa ni George Burley alietunukiwa baada ya kuiwezesha Ipswitch Town ishike nafasi ya 5 Msimu wa mwaka 2000/01.
Tuzo hii ya Meneja Bora hutolewa na Wadhamini wa Ligi Kuu, Barclays, na jopo la uteuzi huwa ni Vyama vya Soka, Vyombo vya Habari na Mashabiki.

No comments:

Powered By Blogger