Sunday 21 December 2008

MAN U NI MABINGWA WA DUNIA! Rooney awapa ushindi!!

Mabingwa wa England na Ulaya, Manchester United, wamejiongezea taji lingine na sasa ni Klabu Bingwa Duniani baada ya kuipachika Liga de Quito ya Ecuador, Mabingwa wa Marekani Kusini, bao 1-0 kwa bao tamu la Wayne Rooney katika mechi ya Fainali ya Klabu Bingwa Duniani iliyochezwa Yokohama, Japan.
Wakiwa wametawala kipindi chote cha kwanza na kukosa mabao mengi, Manchester United walipata pigo pale Beki wao Nemanja Vidic alipotolewa nje kwa Kadi Nyekundu dakika ya 49 ya mchezo baada ya kumpiga kipepsi Mchezaji wa Quito Claudio Bieler.
Ikabidi Man U wamtoe Fowadi Carlos Tevez na kumwingiza Mlinzi Johnny Evans kuziba pengo la Vidic.
Hata hivyo pengo la kucheza watu 10 halikuonekana kwani Man U waliendelea kutawala na kushambulia.
Ilipofika dakika ya 73, kazi nzuri ya Cristiano Ronaldo ilimkuta Wayne Roonel aliefunga bao safi la ushindi.
Meneja Sir Alex Ferguson alikipongeza kikosi chake kwa kucheza kitimu na juhudi hasa walipokuwa 10 tu.
Nae Mchezaji aliewapa Kombe, Wayne Rooney, alietangazwa ndie Mchezaji Bora wa Mashindano, alijigamba: 'Sisi ndio bora duniani! Ushindi huu ni muhimu kwa klabu!'

LIGI KUU ENGLAND: Arsenal 1 Liverpool 1

Vinara wa LIGI KUU ya England, Liverpool walilazimisha sare ya 1-1 na Arsenal katika mechi iliyochezwa nyumbani kwa Arsenal uwanja wa Emirates.
Arsenal walipata bao lao kwenye dakika ya 24 baada ya Robin Van Persie kufunga bao la kifundi sana baada ya kupokea pasi safi toka kwa Samir Nasri.
Liverpool, wakicheza bila ya kuwa na Meneja wao Rafa Benitez aliefanyiwa operesheni kuondolewa vijiwe kwenye figo, walisawazisha kwa bao zuri pia kupitia Robbie Keane aliefumua shuti kali dakika ya 42.
Mshambuliaji nyota wa Arsenal Emmanuel Adebayor alipewa Kadi Nyekundu dakika ya 62 baada ya kupata Kadi 2 za Njano.

Matokeo mechi nyingine za LIGI KUU:

Newcastle 2 Tottenham 1

West Brom 2 Manchester City 1

MECHI INAYOFUATA: Jumatatu, 22 Desemba 2008: Everton v Chelsea

Endapo Chelsea ataifunga Everton kwenye mechi hii, basi Chelsea atachukua uongozi wa LIGI KUU.

Mpaka sasa msimamo kwa Timu 5 za juu ni kama ufuatavywo:

-Liverpool: mechi 18 pointi 39

-Chelsea: mechi 17 pointi 37

-Aston Villa: mechi 18 pointi 34

-Manchester United: mechi 16 pointi 32

-Arsenal: mechi 18 pointi 31

No comments:

Powered By Blogger