Sunday 7 December 2008

Mabingwa Man U washinda kwa mbinde: Beki Vidic apachika bao la ushindi dakika za majeruhi!!!

Goli lililofungwa na Nemanja Vidic, Beki pacha na Rio Ferdinand, kwenye dakika ya 90 ya mchezo, liliwapa ushindi wa bao 1-0 Mabingwa Man U wakiwa nyumbani Old Trafford wakicheza na Sunderland timu ambayo haina Meneja baada ya Roy Keane kuitema na ambayo kwa sasa iko nafasi za mwisho kabisa kwenye msimamo wa LIGI KUU.
Nae Meneja wa Man U, Sir Alex Ferguson, alishuhudia mechi hii akiwa amekaa jukwaani [pichani akiwa amekaa nyuma ya Mkurugenzi na Mchezaji wa zamani wa Man U Sir Bobby Charlton] kwa Watizamaji ikiwa ni kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi 2 na hivyo kutoruhusiwa kukaa benchi la timu yake baada ya kufarakana na Refa Mike Dean wakati Man U ilipocheza na Stoke.
Hii ilikuwa mechi yake ya pili ya kifungo.
Wimbi baada ya wimbi la mashambulizi kwa dakika zote za mchezo hazikuzaa goli kwani Wachezaji karibu wote wa Sunderland walijikita mbele ya penalti boksi yao kujihami.
Wenyewe Wazungu wanaita 'Timu imepaki basi mbele ya mlango wao'.
Katika mechi nzima Man U walipiga jumla ya mashuti 23 golini na Sunderland hawakupiga hata moja.

Man U walipata kona 10 na Sunderland walipata 1 tu na ambayo ndiyo ilisababisha kifo chao.
Kona hiyo pekee waliyopata Sunderland dakika ya 89 ilizuiwa na ukuta wa Man U na huku Wachezaji wengi wa Sunderland wakiwa wamepanda golini kwa Man U ili kuongeza mashambulizi, Man U walifanya shambulizi la haraka na Kiungo Michael Carrick akiwa nje ya boksi alipiga shuti lilombabatiza Collin Edwards, kumpita Kipa, na kugonga posti chini na kurudi ndani na mpira kumkuta Beki Nemanja Vidic aliushindilia wavuni.
Man U walimiliki mpira kwa asilimia 78 na Sunderland asilimia 28 tu!

Wataalam wa LIGI KUU wameielezea mechi hii kuwa ni ya upande mmoja sana kiasi ambacho haijawahi kutokea ingawa cha kushangaza ni kukosekana lundo la magoli.
Katika mechi hii Mabingwa Man U walipata pigo pale Mchezaji wao Bora wa Ulaya Ronaldo alipoumia na ikabidi atoke nje ya uwanja kwenye dakika ya 68.
Ingawa Man U hawakupata ushindi wa kishindo lakini kupata pointi 3 kwao ni jambo bora kwani linawafanya bado wawe karibu sana na vinara wa ligi Liverpool na Chelsea.
Msimamo mpaka sasa ni:
Liverpool: mechi 16 pointi 37
Chelsea: mechi 16 pointi 36
Man U: mechi 15 pointi 31
Arsenal: mechi 16 pointi 29
MECHI ZA LEO:
Jumapili, 7 Decemba 2008
[saa 12 jioni] West Brom v Portsmouth
[saa 1 usiku]Everton v Aston Villa

No comments:

Powered By Blogger