LIGI KUU England: Wabongo wafarijika baada ya DSTV kuokoa jahazi!!!
Tangu wikiendi iliyokwisha, baada ya kukosa kuona matangazo ya moja kwa moja, yaani laivu, ya mechi za LIGI KUU England kufuatia kufilisika kwa Kampuni iliyokuwa ikimiliki GTV waliokuwa na haki ya asilimia 80 kuonyesha mechi za LIGI KUU, Wabongo walikuwa na majonzi makubwa lakini leo wameibuka kidedea na kushangilia kufuatia taarifa rasmi kutoka DStv kuwa wamefanikiwa kupata leseni ya kuonyesha laivu mechi zote za LIGI KUU msimu huu na kazi hiyo wataianza kwa mechi zote za wikiendi hii zitakazoonyeshwa kwenye Chaneli zake za Supersport na vilevile leseni hiyo imewaruhusu kuonyesha mechi zote za msimu ujao.
Awali, DStv walipewa haki ya kuonyesha asilimia 20 tu za mechi za LIGI KUU kwa Nchi za Kusini mwa Sahara, ikiwemo Tanzania, ingawa huko Makao Makuu yao Afrika Kusini na Nigeria walipewa haki ya kuonyesha mechi zote.
Kabla ya kuibuka kwa GTV mwaka uliokwisha, DStv ndio walikuwa pekee wakionyesha mechi zote na walijenga sifa kubwa, umaarufu na uaminifu mkubwa kwa umahiri wao miongoni mwa Washabiki wa Bongo.
FIFA yatangaza Nchi zinazogombea Uenyeji wa Fainali Kombe la Dunia 2018
England, ambae ndie anapewa nafasi kubwa kunyakua Uenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia 2018, atapata upinzani toka kwa Wapinzani 10 wakiwa ni Spain na Portugal, wanaoomba kwa pamoja kuwa Wenyeji kwa kushirikiana, sawa na Uholanzi na Ubelgiji ambao nao watashirikiana.
Nchi zinazoomba kila moja kivyake ni Urusi, Australia, USA, Mexico, Qatar, Indonesia, Japan na Korea.
Ingawa mwaka 2002, Japan na Korea walishirikiana kuwa Wenyeji safari hii kila nchi imeomba kivyake.
Kura ya kumchagua mwenyeji itafanywa na FIFA Desemba mwaka huu.
Mwenyeji wa Fainali zijazo za 2010 ni Afrika Kusini na zile za 2014 zitafanyika Brazil.
Shaun Wright-Phillips ashtakiwa na FA!!!
Chama cha Soka cha England, FA, kimemshtaki Mchezaji wa Manchester City Shaun Wright- Phillips kwa kuleta vurugu mbaya kwenye mechi ya Jumamosi ambayo Man City walifungwa na Stoke.
Shaun Wright-Phillips alibabatizwa na mpira kwa makusudi na Mchezaji wa Stoke Rory Delap wakati filimbi ishalia na Refa Martin Atkinson akampa Kadi Nyekundu Delap lakini hakumwona Shaun Wright-Philips akilipiza kisasi kwa kumpiga teke Delap.
Lakini baada ya mechi, alipoona video ya tukio lote, Refa Martin Atkinson akakiri endapo angeliona tukio hilo basi Shaun Wright-Phillips angepewa Kadi Nyekundu pia.
Shaun Wright-Phillips amepewa hadi kesho Alhamisi saa 3 usiku [bongo taimu] kutoa utetezi wake.
Nao Middlebrough wakiri kosa kwa FA la kushindwa kudhibiti Wachezaji wao!!!
Middlesbrough wamekubali kosa waliloshitakiwa na FA la kushindwa kudhibiti Wachezaji wao kwenye mechi waliyobamizwa 3-0 na West Brom Januari 17 kufuatia vitendo vya Wachezaji wake kumzonga Refa Mark Halsey alipomtoa nje Mchezaji wa Middlesbrough Didier Digard kwa Kadi Nyekundu alipomchezea rafu Borja Valero na kumsababisha Refa huyo adondoshe chini Kadi yake.
Mbali ya kukubali kosa, Klabu ya Middlesbrough imeomba iende mbele ya kikao kitakachotoa adhabu ili iwakilishe ombi la kupunguziwa adhabu.
Tottenham yampa Mchezaji 'mpya' Robbie Keane Unahodha!!!
Meneja wa Tottenham, Harry Redknapp, amemteua Robbie Keane kuwa Nahodha wake mara tu baada ya Mchezaji huyo kununuliwa kutoka Liverpool hapo juzi.
Robbie Keane ndie aliekuwa Nahodha wa Tottenham kabla hajauzwa kwenda Liverpool miezi 6 iliyokwisha.
Harry Redknapp ametamka: 'Nahisi kurudi kwa Keane hapa kutatuletea msukumo mpya! Yeye ni mtu mwenye mvuto mkubwa na kila sifa ya ushujaa na uongozi!!'
Kwa sasa Tottenham iko kwenye patashika ya kujikwamua toka nafasi za mwisho kwenye msimamo wa ligi zinazohatarisha timu kushuka daraja.
No comments:
Post a Comment