Tuesday 24 February 2009

Arsenal v AS Roma na Inter Milan v Manchester United
Wenger alia Arshavin kutocheza, Ferguson asema goli ni muhimu leo na Mourinho adai mshindi atajulikana Old Trafford na si leo!!

Beckham alikuwa na Man U mazoezini San Siro ili kuwapa moyo!!

Leo usiku Arsenal wanajimwaga uwanjani kwao Emirates kupambana na AS Roma ya Italia huku Meneja wao Arsene Wenger akishangazwa na sheria za UEFA zinazomzuia Mchezaji wake mpya Andrei Arshavin kucheza leo kwa vile hapo awali alicheza mashindano haya akiwa na Zenit St Petersburg ambayo kwa sasa haipo tena mashindanoni baada kutolewa nje kwenye Makundi.
Wenger, ambayo Timu yake ina ubutu kufuatia kuumia kwa Washambuliaji kadhaa akiwemo Nyota Adebayor, alilalama: 'Sheria zinashangaza lakini tulipomnunua tulijua hilo!
Nae Mchezaji wa Brazil aliewahi kuchezea Arsenal kwa mkopo akitokea Real Madrid ambae kwa sasa yuko AS Roma, Julio Baptista ametamba wao ndio wanaostahili kushinda leo.
Baptista alikaririwa akisema: 'Sie ndio tunategemewa kushinda! Arsenal wana upungufu mkubwa kwa kuwakosa Fabregas, Adebayor, Eduardo, Walcot na hata Rosicky! Tunajua Arsenal ni hatari bila ya hata hao Wachezaji lakini ukweli kuwakosa hao ni pigo kubwa kwao!'
Huko Milan, Italia, vita ya kisaikolojia iliyojulikana sana wakati Mourinho akiwa na Chelsea, iliendelea tena kati ya Mourinho safari hii akiwa na Inter Milan ambao leo wanakutana na Manchester United uwanjani San Siro huku Mourinho akidokeza mechi ya leo itakuwa suluhu kwa vile Manchester United watajihami ili washinde marudiano yatayochezwa Old Trafford wiki mbili zijazo.
Hata hiyo mechi ya marudiano, Mourinho amedokeza huenda ikaamuliwa katika muda wa nyongeza!
Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, ambayo Timu yake inakabiliwa na uhaba wa Walinzi baada ya Nemanja Vidic kufungiwa mechi hii na kina Wes Brown, Neville, O'Shea na Evans kuwa majeruhi, amekataa maoni ya Morinho na kusisitiza wao wanaingia uwanjani kushinda na kwamba bao la ugenini ni muhimu sana kwao.
Ferguson amesema: 'Man U siku zote hushambulia! Siku zote tunatafuta ushindi!'
Man U leo asubuhi walifanya mazoezi San Siro na David Beckham aliechezea Man U tangu akiwa mtoto na kwa sasa yupo Milan akiwa Timu ya AC Milan wapinzani wakubwa wa Inter Milan, alikuwepo mazoezini kuwapa moyo marafiki zake na aliongea na Wachezaji na Sir Alex Ferguson.
Baada ya mazoezi hayo ya Man U, Beckham alienda Hotelini walikofikia Man U kwa maongezi zaidi.

LIGI KUU England: Hull City 1 Tottenham Hotspurs 2

Beki Jonathan Woodgate alifunga bao kwa kichwa dakika ya 86 na kuipa Tottenham ushindi muhimu ulioifanya kupanda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi wakiwa pointi 5 juu ya timu zilizo kwenye nafasi ya timu zinazo poromoka daraja.
Tottenham walipata bao la awali kupitia Winga Aaron Lennon aliefunga kwa shuti la mita 20 dakika ya 17 lakini Hull City wakiwa kwao KC Stadium walisawazisha dakika ya 27 kupitia Turner.

No comments:

Powered By Blogger