Baada ya miezi miwili ya 'mapumziko' LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA', yaani UEFA CHAMPIONS LEAGUE, inarudi tena dimbani na safari hii zipo jumla ya Timu 16 zikicheza mechi za mtoano, nyumbani na ugenini, kupata Timu 8 zitakazoingia Robo Fainali.
Mechi za kwanza zitachezwa kesho Jumanne na nyingine kesho kutwa Jumatano na marudiano ni wiki mbili baadae.
Ifuatayo ni tathmini na utabiri Timu ipi itaibuka kidedea baada ya mechi mbili:
MANCHESTER UNITED v INTER MILAN
Ni mechi ya kutoa ute kwa mashabiki na hata wale wasiokuwa na upande.
Ni mechi inayokutanisha Mabingwa Watetezi wa Kombe hili na moja ya Timu Bora Italia ingawa haijawahi kushinda Kombe hili tangu mwaka 1965.
Ni mechi ngumu inayowakutanisha tena Sir Alex Ferguson na Jose Mourinho wakikumbushana 'vita vyao' vya tangu Mourinho akiwa FC Porto hadi Chelsea.
Inter Milan ingawa ni Timu ya Italia ina Wachezaji wawili tu toka Italia na imesheheni Wachezaji wa nje hasa Marekani ya Kusini na nguzo yao kubwa ni Washambuliaji wao wenye nguvu Zlatan Ibrahimovic na Adriano huku Man U wakitegemea ufundi, wepesi na ushirikiano wa kina Rooney, Ronaldo, Berbatov, Carrick na kikosi chao kizima.
UTABIRI: MAN U
AS ROMA v ARSENAL
Ni mechi ya Timu zinazocheza 'Soka Tamu' Ulaya ingawa Timu hizi kwenye ligi zao zipo chini ya kiwango na zimo hatarini kushindwa kuingia LIGI YA KLABU BINGWA ULAYA msimu ujao kutokana na kuwa nafasi za chini kwenye ligi za nchini kwao.
Arsenal wanakabiliwa na majeruhi kwa Mastaa wao kama Fabregas, Adebayor na Eduardo na hivyo wana ubutu. Mchezaji mpya Andrei Arshavin haruhusiwi kucheza kwa vile aliichezea Timu yake ya zamani Zenit St Petersburg awali kwenye Kombe hili.
Nguzo ya AS Roma ni, bila shaka, Francesco Totti na kwa sababu mechi ya kwanza inachezwa uwanja wa AS Roma Olympic Stadium, Totti atawika na hili ni tatizo kubwa kwa Arsenal.
UTABIRI: AS ROMA
FC BARCELONA v LYON
Kwa sasa, wachezesha kamari wote wa Ulaya wanawapa Barcelona nafasi ya kwanza kutwaa Ubingwa huu huku Mabingwa Watetezi Manchester United wakipewa nafasi ya pili.
Hilo ndio tatizo kubwa kwa Lyon ingawa wanae Mchezaji nyota na kipaji kikubwa Karim Benzema.
UTABIRI: BARCELONA
FC PORTO v ATLETICO MADRID
Kimaandishi Atletico Madrid wangestahili kushinda mpambano huu lakini Atletico Madrid wana migogoro na walimtimua Meneja wao huku Mastaa wao Diego Forlan na Sergio Aguero viwango vyao vimeshuka mno.
FC Porto nyumbani kwao Ureno ni wababe na hawajafungwa hata mechi moja tangu Novemba mwaka jana.
UTABIRI: FC PORTO
LIVERPOOL v REAL MADRID
Hili, kama lile la MAN U v INTER MILAN, ni pambano linalotoa udenda kwa mashabiki na vyombo vya habari.
Hili ni pambano ambalo unahitaji 'Mtabiri wa Kulipwa' ili utabiri nani atashinda!
Real wanaongozwa na Meneja Mhispania Juande Ramos aliefukuzwa kazi hivi karibuni huko England alipokuwa na Tottenham.
Liverpool inaongozwa na Meneja Mhispania Rafael Benitez.
Hii ni vita ya Spain!
UTABIRI: REAL MADRID
JUVENTUS v CHELSEA
Baada ya MAN U v INTER MILAN, hii ni mechi ya pili baina ya ENGLAND v ITALY!
Wakati Juventus ikiendeleza mapambano yake bila ya sokomoko lolote chini ya Meneja Claudio Ranieri aliekuwa Meneja wa kwanza wa Chelsea kutimuliwa na Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovic mwaka 2004, Chelsea wanaingia vitani ikiwa ni mechi ya pili tu tangu Meneja mpya Guus Hiddink apewe wadhifa baada ya kufukuzwa Mbrazil Luiz Felipe Scolari.
Kuyumba kwa Chelsea kunaipa matumaini Juve ya Mchezaji Mkongwe Alessandro Del Piero.
UTABIRI: JUVENTUS
BAYERN MUNICH v SPORTING LISBON
Ndiyo ni mechi ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE lakini kwa vyovyote vile haiwezi kushika bango kubwa Ulaya kote na duniani kote!
Wengi wanaamini mbali ya Bayern Munich kumkosa Mshambuliaji wao mkuu Luca Toni alieumia, waliobaki kina Miroslav Klose, Franck Ribery na Lucas Podolski ni bunduki tosha kwa Meneja wao Jurgen Klinsman kushangilia ushindi!
UTABIRI: BAYERN MUNICH
PANATHINAIKOS v VILLAREAL
Hizi ni Timu mbili zisizo na ubavu kuwa Mabingwa wa Ulaya lakini ondoa shaka zina uwezo wa kumtetemesha hata huyo atakaechukua Ubingwa kwani ni Timu ngumu kufungika.
Villareal waliweza kuwasimamisha Mabingwa Watetezi Man U kwenye mechi mbili za Makundi awali kwenye Kombe hili na kutoka sare ya bila kufungana.
Nao Panathinaikos, kwenye Makundi, waliwabamiza Inter Milan iliyokuwa kwake San Siro na kumaliza wakiwa juu yao kwenye msimamo wa Makundi.
Lakini Villareal wakiwa na Mkongwe wa Arsenal Robert Pires na Chipukizi alietokea Man U Giussepe Rossi wana uwezo wa kuwabwaga hao Wagiriki.
UTABIRI: VILLAREAL
No comments:
Post a Comment