Monday, 19 October 2009

SAKATA LA ‘GOLI LA PUTO JEKUNDU’: Ligi Kuu yasema mechi ya Sunderland na Liverpool hairudiwi!!!
Ligi Kuu England imetamka kuwa mechi ya Sunderland na Liverpool ambayo Liverpool alifungwa 1-0 kwa bao la Darrent Bent dakika ya 5 ya mchezo baada ya kufumua shuti lililougonga ‘mpira wa bichi’ uliotupwa uwanjani na Shabiki wa Liverpool na kisha kumbabaisha Kipa wa Liverpool Pepe Reina na kutinga wavuni haiwezi kurudiwa licha ya ukweli kuwa Refa Mike Jones alifanya kosa kubwa kulikubali goli hilo.
Kufuatana na Sheria za mpira ilitakiwa Refa akatae goli hilo kwa vile mchezo uliingiliwa na kitu toka nje na kisha alitakiwa aamue mpira udondoshwe kati ya Wachezaji wawili, mmoja wa Sunderland na mwingine wa Liverpool, ili kuuanzisha tena mchezo.
Msemaji wa Ligi Kuu amesema haiwezekani mechi hiyo kurudiwa kwa vile FIFA inaamini na kufuata ile desturi kuwa ‘uamuzi wa Refa ni wa mwisho.’
Hata hivyo, FIFA, miaka minne iliyopita yenyewe ilienda kinyume na hiyo desturi yao pale ilipoamuru mechi ya Mtoano wa Kombe la Dunia kati ya Uzbekistan na Bahrain irudiwe baada ya kugundulika Refa alifanya kosa kwa kulikataa goli walilofunga Uzbekistan kwa penalti na kuamua Baharain wapige frikiki wakati uamuzi sahihi ulikuwa ni kuamua penalti ipigwe tena.
Mbali ya kuonekana wameonewa, Klabu ya Liverpool haina mpango wa kushika bango mechi irudiwe na hata Meneja wao Rafa Benitez amekiri kuwa ni suala la kiufundi ingawa inawezekana hakujua kuwa kisheria lile goli halikuwa halali.
Nae Steve Bruce, Meneja wa Sunderland, amekubali kuwa alikuwa hajui kama kisheria lile goli si halali lakini amesema mara nyingine maamuzi huenda kinyume nao.
Owen: “Sikuisaliti Liverpool kwa kujiunga Man U!!”
Mchezaji wa Manchester United Michael Owen amekubali kuwa atapata wakati mgumu sana Jumapili ijayo pale Timu yake itakapokwenda Anfield kucheza mechi ya Ligi Kuu na Wapinzani wao wa jadi Liverpool, Klabu ambayo ndiyo alianza kuichezea.
Huku akisisitiza yeye si msaliti, Michael Owen alisema: “Nikicheza na kufunga goli ntashangilia kama kawaida! Lazima wakubali mie ni binadamu. Ningependa watu watambue mchango wangu kwao nilipochezea Liverpool na watambue kuwa sasa nipo kwa Mahasimu wao Man U na nitacheza kwa nguvu zote!”
Owen ameendelea kueleza: “Watu wanazungumzia uaminifu na kwa Shabiki ni rahisi kuzungumzia hilo! Lakini mie ni Baba, Kaka na Mtoto na ni Mchezaji ambae anatafuta kula yake na ailishe Familia yake! Nilipokuwa mtoto niliishabikia Everton wapinzani wa Liverpool lakini sikuchezea Everton na nikachezea Liverpool! Nimechezea Real Madrid na mie si Shabiki wa Real! Hii ni kazi kama kazi nyingine!”
Hughes anaamini “BIGI 4” msimu huu watakwama!!!!
Mark Hughes ambae ni Meneja wa ‘Timu Tajiri’ Manchester City amesema anaamini hao wanaoitwa “BIGI 4”, yaani Manchester United, Chelsea, Liverpool na Arsenal ambao wamekuwa wakiitawala Ligi Kuu miaka ya hivi karibuni, msimu huu watakwama na kufungwa na Timu nyingine.
Mpaka sasa msimamo wa Ligi Kuu ni kama ufuatavywo:
1. Manchester United mechi 9 pointi 22
2. Chelsea mechi 9 pointi 21
3. Tottenham mechi 9 pointi 19
4. Arsenal mechi 8 pointi 18
5. Man City mechi 8 pointi 17
6. Aston Villa mechi 8 pointi 16
7. Sunderland mechi 9 pointi 16
8. Liverpool mechi 9 pointi 15
Mark Hughes amesema: “Unaweza kuhisi msimu huu hao ‘BIGI 4’ wanafungika! Hili ni nzuri kwa ligi! Wameshapoteza pointi nyingi mwanzoni na watapoteza nyingi tu!”

No comments:

Powered By Blogger