Tuesday 20 October 2009

BAADA YA GOLI LA PUTO [Mpira wa Bichi]:
Washabiki wa Man U kusachiwa, kunyang’anywa Mipira ya Bichi Anfield Jumapili ijayo!!!
Jumapili ijayo huko Uwanjani Anfield, Mashabiki wa Manchester United ambao wataingia uwanjani kwenda kushuhudia pambano la Ligi Kuu baina ya Liverpool na Manchester United watalazimika kusachiwa na kunyang’anywa Mipira ya Bichi ili kuwazuia wasishangilie kwa kebehi na pengine kusababisha goli kama alilofunga Mshambuliaji wa Sunderland Darren Bent Jumamosi iliyopita pale Liverpool walipopigwa 1-0 baada ya mpira kuugonga mpira wa bichi uliotupwa uwanjani na Shabiki wa Liverpool na kumhadaa Kipa Pepe Reina.
Wakati huo huo, Polisi wamesema wanalichunguza tukio hilo la kurushwa mpira huo wa bichi uwanjani na mpaka sasa hawajamtambua Kijana alieurusha ingawa picha yake ilionekana waziwazi kwenye mikanda ya video.
Pia kuna taarifa kuwa Washabiki wa Liverpool wameonyesha chuki na hata kutoa vitisho kwa Kijana huyo alierusha mpira huo wa bichi ingawa nae pia ni Shabiki wa Liverpool.
Lakini baadhi ya watu wamemtetea Kijana huyo na kusema ingawa hakupaswa kurusha mpira huo wa bichi lakini alipourusha Kipa Pepe Reina aliuona na kuutoa nje ya uwanja nyuma ya goli lakini ulitulia dakika chache na kupeperushwa tena uwanjani na ndipo shuti la Darren Bent likaubabatiza na kumwacha Reina akitaka kudaka mpira huo wa bichi mwekundu huku mpira riali ukitinga wavuni.
JANA LIGI KUU: Fulham 2 Hull City 0
Kwenye mechi pekee ya Ligi Kuu hapo jana usiku, Fulham ikiwa nyumbani Craven Cottage imeitwanga Hull City mabao 2-0.
Mabao ya Fulham yamefungwa na Bobby Zamora dakik 2 kabla haftaimu baada ya shuti la Damien Duff kutemwa na Kipa Boaz Myhill na la pili alifunga Diomansy Kamara baada ya pande tamu la Zamora.
Kwa ushindi huo, Fulham imejinasua toka Timu 3 za mwisho na sasa wako nafasi ya 12 wakiwa na pointi 10 na Hull City bado wamejikita kwenye nafasi 3 za mwisho.

No comments:

Powered By Blogger