Vinara wa LIGI KUU Chelsea na Liverpool leo wanajimwaga viwanjani huku macho ya wengi yakitazama kama Steven Gerrard wa Liverpool na Frank Lampard wa Chelsea watacheza baada ya kujitoa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Uingereza iliyoifunga Ujerumani katika mechi ya kirafiki mabao 2-1 siku ya Jumatano mjini Berlin, Ujerumani.
Wachezaji hao walijitoa kwa madai ni majeruhi na kitendo hicho kilimkera Meneja wa Uingereza Fabio Capello na akalazimisha Wachezaji hao waende kwenye kambi ya Timu ya Uingereza ili wachunguzwe na Madaktari wa timu hiyo.
Leo Chelsea inawakaribisha Stamford Bridge Newcastle ambao hawajawahi kushinda hapo katika mechi za LIGI KUU.
Liverpool nao wanawakaribisha Fulham uwanjani Anfield ambako katika mechi 7 za LIGI KUU walizocheza hapo, Fulham hawajashinda hata moja na wameweza kufunga bao 2 tu.
Mabingwa wa LIGI KUU, Man U, ambao wako nafasi ya 3 nyuma ya Chelsea na Liverpool, wanashuka uwanjani Villa Park kucheza na wenyeji wao Aston Villa ambao wako nafasi ya 5.
Man U aliecheza mechi moja pungufu ana pointi 24 akifuatiwa na Arsenal na Aston Villa wenye pointi 23.
Aston Villa, ambao waliwabamiza Arsenal mabao 2-0 huko Emirates Stadium katika mechi iliyokwisha, hawajawahi kuwafunga Man U katika mechi 11 zilizopita.
Huenda leo Man U ikamkosa Dimitar Berbatov alieumia siku ya Jumatano wakati akiichezea Timu yake ya Taifa ya Bulgaria ilipocheza na Serbia ingawa Wachezaji Rio Ferdinand na Wayne Rooney waliokosa mechi ya wiki iliyopita ya ushindi wa 5-0 dhidi ya Stoke City wanaweza kuwemo dimbani.
Manchester City leo watawakaribisha Arsenal ambao wako kwenye kipindi kigumu sana hasa baada ya kufungwa mabao 2-0 nyumbani Emirates na Aston Villa wiki iliyopita, kisha kumpoteza nyota chipukizi Theo Walcott alepasuliwa bega na jana Klabu ilithibitisha haina Nahodha baada ya Nahodha William Gallas kutimuliwa kwa kuanika 'chupi chafu' hadharani!
No comments:
Post a Comment