Saturday, 11 July 2009

Mchezaji wa Man City akwaa ‘Mafua ya Kitimoto’, akwama Cyprus!!!
Mchezaji wa Timu ya England na Klabu ya Manchester City, Micah Richards, umri miaka 21, amezuiwa kuondoka Kisiwa cha Cyprus alikokuwa mapumzikoni baada ya kuupata ugonjwa wa ‘Mafua ya Nguruwe’ na sasa anaendelea na matibabu.
Richards, ambae amepewa dawa ya Tamiflu ili kuutibu ugonjwa huo, anaelezea: ‘Kwanza nilidhani ninaumwa kifua au nimepata sumu kutokana na pombe nyingi kwani nilikuwa siwezi kuinuka na hata kula! Nilipoambiwa nina ‘Mafua ya Nguruwe’ nilistuka! Unaskia watu wanakufa kwenye Taarifa za Habari!’
Inategemewa Jumapili ataruhusiwa kuondoka kurudi England.
Richards mwenyewe anasema akirudi mazoezini bila shaka Wachezaji wenzake watamletea vitimbwi na mzaha mwingi! Richards anasema: ‘Najua wengine watakuja mazoezini wamejiziba sura kama Madaktari wako kwenye opersheni!’
Man City wakiri kushindwa na Eto'o!!
Manchester City wamekiri kushindwa kumchukua Eto’o kutoka Barcelona na wametamka hawajishughulishe tena kuhusu suala hilo. Man City na Barca zilikuwa zikijadiliana juu ya Mshambuliaji huyo kutoka Cameroun ili ahame kwa Pauni Milioni 25.
Bosi Mkuu wa Man City, Garry Cook, amekiri: ‘Dili imeshindikana!’ Inaelekea kuna utata kuhusu mkataba wa Eto’o na Barcelona ambae alijiunga Barca mwaka 2004 kutoka Mallorca kwa Pauni Milioni 16 na mpaka sasa ameshaifungia Klabu hiyo mabao zaidi ya 100.
Mpaka sasa Man City imeshawanunua Mshambuliaji Roque Santa Cruz kutoka Blackburn kwa Pauni Milioni 18 na Kiungo Gareth Barry kutoka Aston Villa kwa Pauni Milioni 12.
Alonso bado anawindwa na Real, Fabregas hayumo kwenye ‘Listi ya Manunuzi!’
Real Madrid wamesema bado wana nia ya kumnunua Kiungo Xabi Alonso kutoka Liverpool ingawa inasemekana Liverpool wamepandisha dau lake hadi Pauni Milioni 50.
Mkurugenzi wa Michezo wa Real, Miguel Pardeza, ametamka: ‘Real haiachi kufuatilia kitu hadi tujue hakiwezekani. Mpaka sasa kuna vipingamizi lakini tunaweza kubadilisha hilo.’
Hata hivyo, Pardeza amekanusha taarifa kuwa bado wanamtaka Nahodha wa Arsenal Cesc Fabregas kwa kusema hayumo katika ‘Listi yao ya Manunuzi’.
Mdau Kroenke aongeza hisa Arsenal!
Mkurugenzi wa Arsenal Stan Kroenke, mwenye hisa nyingi Klabuni Arsenal, ameongeza hisa zaidi na sasa anamiliki karibu aslimia 29 ya hisa zote na kumfanya akaribie hisa za aslimia 30 ambazo, kisheria, zitamlazimisha atoe ofa ya kununua hisa zote Klabuni hapo.
Kroenke, ambae ni Mmarekani anaemiliki Klabu ya Mpira wa Vikapu ya NBA Denver Nuggets, Klabu ya Mpira wa Magongo Colorado Avalanche na Klabu ya Soka ya Colorado Rapids zote za Marekani, mwezi Mei alinunua hisa nyingine na kumpiku Mrusi Alisher Usmanov kama mtu mwenye hisa nyingi.
Hivi karibuni kumekuwa na mvutano katika Bodi ya Arsenal huku Mdau Usmanov akitaka Wenger apewe fedha nyingi kununua Wachezaji lakini Bodi ikagoma.
Jermaine Pennant ahamia Zaragoza!
Winga wa Liverpool, Jermaine Pennant, aliekuwa akichezea Portsmouth kwa mkopo sasa amehamia Real Zaragoza baada ya mkataba wake na Liverpool kumalizika mwanzoni mwa mwezi huu.
Pennant pia alipata ofa kujiunga na AC Milan lakini akaikataa kwa sababu anaelewa Klabu hiyo itamchukua David Beckham na hivyo kumfanya akose namba ya kudumu.
Real Zaragoza iliyokuwa Daraja la chini msimu huu imerudi tena Daraja la juu La Liga.

No comments:

Powered By Blogger