Wednesday 20 January 2010

Carling Cup: Kipigo cha mechi ya kwanza, Fergie hajavunjika moyo, aahidi kisago Old Trafford!!!
• Refa kuibeba Man City, Fergie asema: “Kila mtu kaona!!”
Sir Alex Ferguson amegoma kuvunjika moyo kufuatia kipigo cha 2-1 hapo jana katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling iliyochezwa nyumbani kwa Mahasimu wao Manchester City Uwanjani City of Manchester ambako Carlos Tevez alipachika bao 2 na kuwapa ushindi.
Marudiano ni wiki ijayo huko Old Trafford siku ya Jumatano Januari 27.
Fergie amesisitiza: “Tutacheza nyumbani! Itakuwa ni ujinga ikiwa hujipi matumaini kwani tutakuwa ndani ya Uwanja wetu, mbele ya Mashabiki wetu na wao ni Mahasimu wetu na kila Mchezaji wetu anajua hilo!!”
Fergie akazungumzia mechi ya jana na kusema: “Tulicheza vizuri na tulitawala mchezo! Waliposawazisha tiulipoteana kwa robo saa hivi kisha tukatawala kabisa!!”
Kuhusu Tevez, ambae alikuwa Man U kabla kwenda Man City, kufunga bao zote mbili, Ferguson amesema: “Hilo ni soka!! Kuna Wachezaji wengi wamehama kwetu na wakaja kutufunga! Sisi tunaridhika na Wachezaji wetu!”
Katika mechi ya jana, Manchester United ndio walipata bao la kwanza kupitia Ryan Giggs lakini Manchester City wakasawazisha dakika mbili kabla haftaimu baada ya Refa Mike Dean kuwapa penalti wakati rafu yenyewe ilichezwa wazi kabisa nje ya boksi wakati Beki wa Man U Rafael alipomvuta jezi Bellamy.
Tevez alifunga penalti hiyo na kipindi cha pili Tevez tena akafunga bao la pili kwa kichwa dakika ya 65 kufuatia kona.
Ferguson alikataa kuzungumzia kwa undani kuhusu Refa Mike Dean kuwabeba Man City na akasema kwa mkato: “Sizungumzii hilo! Kila mtu aliona mwenyewe!! Leo maamuzi hayakuwa kwetu, siku nyingine yatakuwa kwetu!!”

No comments:

Powered By Blogger