LIGI KUU: Aston Villa 0 West Ham 0
Uwanja wa Villa Park leo umeshindwa kumpata mbabe katika mechi ya Ligi Kuu England kati ya Wenyeji Aston Villa na West Ham baada ya Timu hizi kutoka sare 0-0.
Kila Timu ilikosa mabao kadhaa ingawa hamna hata moja iliyotawala kabisa mchezo huo.
Katika mechi nyingine iliyoanza muda si mrefu uliopita kati ya Blackburn na Fulham mpaka sasa dakika ya 25 Blackburn wanaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Beki Christopher Samba sekunde chache zilizopita.
Mancini hana ugomvi na Robinho!
Bosi wa Manchester City Roberto Mancini amesisitiza Robinho bado anahitajika na Klabu hiyo licha ya kutokucheza vizuri na jana kulazimishwa kutolewa ingawa aliingizwa kumbadilisha mtu katika mechi ya Ligi Kuu waliyofungwa na Everton 2-0.
Katika mechi hiyo ya jana iliyochezwa Goodison Park, Robinho alikuwa benchi na ilibidi aingizwe dakika ya 8 tu ya mchezo baada ya kuumia kwa Roque Santa Cruz lakini alivurunda vibaya na ilibidi atolewe dakika ya 60 ya mchezo na nafasi yake ichukuliwe na Shaun Wright-Phillips.
Kitendo hicho kilimkera Robinho na alipobadilishwa tu hakuenda kukaa benchi kama ilivyo kawaida bali alienda moja kwa moja vyumba vya kubadilisha jezi.
Mancini ametamka: “Huo si mwisho wa Robinho! Ni Mchezaji mzuri lakini katika Timu hii kila mtu ni lazima afanye bidii na kucheza vizuri!”
Mancini akaongeza katika mechi hiyo na Everton kulikuwa na Mafowadi wengi kina Bellamy, Benjani na Tevez na ilibidi amtoe Robinho.
Robinho alijiunga na Man City mwezi Agosti 2008 akitokea Real Madrid kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 32.5 ambayo ni rekodi Uingereza lakini tangu Mei 2009 hajaifungia Man City hata bao moja.
Hivi karibuni kumekuwa na uvumi kuwa Barcelona itamchukua Robinho.
Mbiu ya kufukuzwa Rafa yapulizwa kwa nguvu!!
• Murphy asema hafai, aondoke!!!
Danny Murphy, Kiungo wa zamani wa Liverpool ambae sasa ni Mchezaji wa Fulham ingawa yeye mwenyewe anadai ni Shabiki wa kutupwa wa Liverpool, amesema maendeleo ya Klabu hiyo yamerudi nyuma tangu aondoke huko mwaka 2004.
Murphy, miaka 32, amesema sasa umefika wakati wa kumtimua Rafa Benitez kwa sababu anaipeleka Klabu hiyo pabaya.
Murphy amehoji kuwa licha ya kuruhusu Alonso aondoke inashangaza kuona pia akiwauza kina Crouch na Bellamy na sasa anamtegemea mtu mmoja tu na ambaye ni Torres.
Murphy amefoka: “Timu hii sasa inategemea watu watatu tu na ni Torres, Gerrard na Carragher! Katika miaka miwili sasa, amefanya maumuzi mabaya mengi ingawa historia inasema alitwaa Ubingwa wa Ulaya na FA Cup! Kwa muda aliokaa Liverpool, sasa hivi ilitakiwa watu waulize Ubingwa wa Ligi Kuu unakuja au la na si watu kugombea kumaliza katika 4 bora na kuingia UEFA CHAMPIONS LEAGUE tu! Na huo Ubingwa hamna Msimu huu! Ni wazi lazima aondoke!”
No comments:
Post a Comment