KOMBE LA AFRIKA: Burkina Faso v Ghana
Mjini Luanda, Uwanja wa Novemba 11, Ghana leo watajitupa na Burkina Faso ili kuwania nafasi ya kuungana na Ivory Coast toka Kundi B kuingia Robo Fainali.
Lakini baada ya kupigwa 3-1 na Ivory Coast, Ghana hawana njia ila lazima waifunge Burkina Faso ili wasonge mbele.
Burkina Faso, baada ya kutoka droo 0-0 na Ivory Coast, wao sare tu inawatosha kusonga mbele.
Kundi hili limebakiwa na Timu 3 tu kufuatia kujitoa kwa Togo baada ya kupata maafa makubwa ya kushambuliwa risasi kwa Basi lao na kuwaua Kocha Msaidizi na Afisa Habari wao pamoja na Dereva wa Basi hilo walipokuwa njiani kwenda Cabinda.
Mbali ya lazima kupata ushindi tu, Ghana wana matatizo Kambini kwao kufuatia kuumia kwa Nyota wao Michael Essien na Wachezaji kadhaa wengine wakiwa kwenye hati hati.
CARLING CUP: Manchester kuwaka moto leo!!!
Jiji la Manchester leo litakuwa ndani ya hekaheka kubwa kufuatia mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Kombe la Carling kuchezwa leo usiku kuanzia saa 5 saa za bongo huko City of Manchester Stadium kati ya Wenyeji Manchester City na Manchester United.
Timu hizi zitarudiana Old Trafford wiki ijayo tarehe 27 Januari.
Hii ni mechi ya 153 kuwakutanisha Mahasimu hao na Man U wameshinda mechi 62, Man City mechi 41 na suluhu 49.
Mara ya mwisho kwa Timu hizi kupambana ilikuwa ni kwenye Ligi Kuu mwanzoni mwa Msimu huu huko Old Trafford na Man U walishinda 4-3.
West Ham yapata Wamiliki wapya!!
David Gold na David Sullivan, ambao waliwahi kuimiliki Klabu ya Birmingham, wameinunua Klabu ya West Ham kwa dau la Pauni Milioni 105.
Ingawa habari hizi hazijathibitishwa rasmi na West Ham lakini duru za karibu ya Klabu hiyo zimehakikisha ukweli wa taarifa hizo na pia kudai kibarua cha Meneja wa Timu hiyo, Gianfranco Zola, kipo salama.
No comments:
Post a Comment