Saturday 23 January 2010

KOMBE LA FA: Muuaji wa Man U aitoa nishai Spurs!!
Jermaine Beckford ambae ndie aliefunga bao moja na la ushindi lililoitupa nje ya FA Cup Manchester United leo tena ameibuka shujaa wa Leeds United alipowafungia mabao mawili huko White Hart Lane na kulazimisha sare ya 2-2 na Wenyeji wao Tottenham Hotspurs kwenye mechi ya Raundi ya 4 ya Kombe la FA.
Mwanzoni mwa mechi hii, Tottenham walikosa kufunga penalti iliyopigwa na Jermaine Defoe na kuokolewa na Kipa wa Leeds Ankergren.
Peter Crouch aliwapa uongozi Tottenham alipofunga bao la kwanza dakika mbili kabla ya mapumziko lakini Leeds wakasawazisha kipindi cha pili dakika ya 52 kupitia mashine yao ya magoli Jermaine Beckford.
Tottenham wakapata bao la pili kupitia Mchezaji alietoka benchi la akiba Roman Pavlyuchenko dakika ya 74 na kuifanya gemu kuwa 2-1.
Ndipo dakika 90 zikakatika na kukaongezwa dakika 5 na ndipo kwenye dakika ya 94 pasi ndefu ikamkuta shujaa Jermaine Beckford ndani ya boksi aliekontroli vizuri na kumchomoka Beki Dawson ambae akamkata Beckford na Refa Alan Wiley hakusita kutoa penalti.
Beckford akafunga penalti hiyo na sasa mechi hiyo itabidi irudiwe nyumbani kwa Leeds Uwanjani Elland Road hapo tarehe 2 Februari.

No comments:

Powered By Blogger