Sunday, 17 January 2010

KOMBE LA AFRIKA: Leo ni leo kwa Cameroun!!!
Cameroun leo wanashuka Uwanja wa Taifa wa Tundavala Mjini Lubango kukwaana na Chipolopolo huku wakiwa wamejeruhiwa baada ya kupigwa kigoli kimoja na Gabon katika mechi ya kwanza.
Zambia wao walitoka sare ya 1-1 na Tunisia.
Hivyo, ili kuhakikisha wana nafasi ya kusonga mbele, Cameroun lazima washinde leo na Kocha wa Cameroun, Mfaransa Paul Le Guen, amesema Timu yake itakuwa makini mno ili kuhakikisha ushindi.
Kocha wa Zambia, Herve Renard, amesema Wachezaji wake watasimama imara mbele ya Cameroun.
Katika mechi ambayo itaitangulia ile ya Cameroun na Zambia hapo Uwanja wa Taifa wa Tundavala, Gabon wanacheza na Tunisia na ushindi kwa Gabon utawapeleka Robo Fainali.
Gabon waliinyuka Cameroun 1-0 katika mechi ya kwanza na Tunisia walienda sare 1-1 na Zambia.
KOMBE LA AFRIKA: Misri yatinga Robo Fainali
Mabingwa Watetezi wa Afrika, Misri, wameingia hatua inayofuata ya Kombe la Afrika baada ya kushinda mechi yao ya pili katika Kundi lao walipoifunga Msumbiji mabao 2-0 hapo jana.
Mabao ya Misri yalifungwa na Dario Khan wa Msumbiji aliejifunga mwenyewe kufuatia krosi ya Ahmed Fathi na la pili alifunga Gedo kwa fataki kali aliyoipiga nje ya boksi.
Mechi ya mwisho ya Misri ni Jumatano watakapocheza na Benin huku Nigeria wakimaliza na Msumbiji.

No comments:

Powered By Blogger