Wednesday 20 January 2010

Soka England leo:
LIGI KUU: Arsenal wanataka kukaa kileleni!!!
MECHI ZA LEO:
Arsenal v Bolton
Liverpool v Tottenham
Ndani ya siku 3, Arsenal wanakutana tena na Bolton baada ya kuwafunga huko kwao mabao 2-0 siku ya Jumapili na leo wapo nyumbani Emirates Stadium na ushindi wa mabao mawili utawapa Arsenal uongozi wa Ligi Kuu na kuzipiku Manchester United na Chelsea.
Msimamo [Timu zimecheza mechi 21 isipokuwa inapotajwa]
1 Chelsea pointi 48
2 Man Utd pointi 47 [mechi 22]
3 Arsenal pointi 45
4 Tottenham pointi 38
5 Man City pointi 38
Katika mechi ya pili ya Ligi Kuu ya leo, Liverpool wanawakaribisha Tottenham na hii ni mechi ngumu mno kwa Liverpool hasa kwa vile itawakosa Mastaa wao Steven Gerrard na Fernando Torres ambao ni majeruhi.
CARLING CUP: Marudiano ya Nusu Fainali Aston Villa v Blackburn
Leo huko Villa Park, nyumbani kwa Aston Villa, Blackburn wanarudiana na Aston Villa na wanawania kulipiza kisasi baada ya kufungwa kwao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe la Carling uliochezwa wiki iliyopita.
Mshindi wa leo atatinga Fainali kukutana na Mshindi wa Manchester United au Manchester City hapo Februari 28.
Blackburn, ambao wanasota chini kwenye msimamo wa Ligi Kuu, pia walitolewa nje na Aston Villa kwenye Kombe la FA.
Mechi hii itaanza saa 4 dakika 45 usiku saa za bongo.
KOMBE LA AFRIKA leo: Nani kuungana na Misri Robo Fainali?
Leo kuna mechi mbili za Kundi C, Misri v Benin na Msumbiji v Nigeria, zitakazoanza kwa pamoja saa 1 usiku hizi zikiwa ndizo mechi za mwisho za Kundi hili huku tayari Misri ashaingia Robo Fainali na pia kujihakikishia kuwa yeye ni Mshindi wa kwanza wa Kundi.
Ili Nigeria afuzu kuingia Robo Fainali wanahitaji sare tu dhidi ya Msumbiji ambao wao ni lazima washinde ili wajipe matumaini ya kusonga .
Ili Benin wasonge mbele kwanza ni lazima waifunge Misri kisha waombe Mungu Nigeria wafungwe na Msumbiji.

No comments:

Powered By Blogger