Monday 3 November 2008


Arsenal walia!!!!

Klabu ya Arsenal, inayosifika kwa kutandaza 'soka zuri', imegubikwa na majonzi makubwa kufuatia mwendo wa kusuasua kwenye LIGI KUU hasa baada ya kupoteza mechi kadhaa kutoka kwa 'vibonde'.
Arsenal wameshafungwa na Hull City na Stoke City timu ambazo zimepanda daraja msimu huu.
Kufungwa huko pamoja na kuimwaga mechi ya Jumatano iliyopita walipocheza na majirani na mahasimu wao wakubwa Tottenham wakati wakiongoza mabao 4-2 huku zikiwa zimesalia dakika mbili tu za mchezo tena wakiwa Uwanja wa nyumbani wa Emirates ndiko kulikoleta simanzi, majonzi na sasa nyufa za kutojiamini zimeanza kuonekana.
Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger. baada ya kufungwa na Stoke City 2-1, alikiri kuwa timu ina udhaifu mkubwa wa kucheza mipira ya juu inayodondoshwa golini kwao. Katika mechi hiyo, 'speshalisti' wa mipira ya kurusha, Rory Delap wa Stoke City, ndie aliesababisha magoli yote baada ya mipira yake ya kurusha kumaliziwa na wenzake.
Baada ya mechi na Tottenham nyota wa Arsenal Emmanuel Adebayor alikubali kuwa kwa 'mtaji huo' klabu yake haiwezi kuchukua ubingwa.
Sasa Nahodha wa timu, William Gallas, amejitokeza kwa kudai ili washinde ni bora Arsenal waachane na kucheza 'soka zuri' badala yake wagangamale kutafuta ushindi.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mchezaji mwingine wa Arsenal beki Gael Clichy aliesema wakati mwingine si vyema kucheza pasi tu ni bora pia kubutua mipira ili kulinda ushindi.
Wiki hii ni wiki muhimu sana kwa Arsenal kwani Jumatano wanacheza kwenye michuano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE watakaporudiana na Fenerbahce ya Uturuki uwanjani Emirates.
Kwenye mechi ya kwanza, Arsenal aliishinda Fenerbahce mabao 5-2 huko Uturuki.
Kisha, Jumamosi, kwenye LIGI KUU, Arsenal watawakaribisha Mabingwa wa LIGI KUU, Man U, uwanjani Emirates.
Kwenye LIGI KUU, Arsenal wanashika nafasi ya 4 wakiwa na pointi 20 kwa mechi 11, Man U wako juu yao nafasi ya 3 wakiwa na pointi 21 ingawa wamecheza mechi moja pungufu [wamecheza 10 tu].

No comments:

Powered By Blogger