Friday 19 September 2008


LIGI KUU YAPAMBA MOTO:


  • LIVERPOOL WAKWAA KISIKI CHA VIBONDE!!

  • ZOLA AANZA VYEMA: TIMU YAKE WEST HAM YASHINDA!!

  • BLACKBURN 1 FULHAM O

Baada ya kuwafunga Mabingwa wa LIGI KUU Man U wiki iliyopita leo uwanjani kwake Anfield Liverpool walikwama kuifunga timu 'kibonde' Stoke City iliyopanda daraja msimu huu kwa kulazimishwa sare ya 0-0. Liverpool, wakiwa na kikosi kamili wakiwemo Nahodha Steven Gerrard na Mshambuliaji staa Fernando Torres, walilazimisha wimbi baada ya wimbi la mashambulizi lakini Stoke City walisimama imara. Liverpool walipata kona zaidi ya 20 lakini zote hazikufua dafu! Hata pale walipofunga goli ambalo wengi walidhani ni halali kabisa Refa alilikataa.
Gianfranco Zola akishika hatamu kwa mara ya kwanza kama Meneja wa West Ham alishuhudia timu yake ikiifunga timu isiyo na Meneja Newcastle kwa bao 3-1. Newcastle kwa sasa inaongozwa kwa muda na aliekuwa msaidizi Chris Houghton baada ya Kevin Keagan kujiuzulu alipokasirishwa na menejimenti kuuza wachezaji bila kumhusisha. West Ham ilipata goli mbili za kwanza kupitia Mtaliana David de Michele na la tatu alilitengeneza Mtaliana huyo huyo kwa kumpasia Matthew Etherington aliefunga.
Michael Owen aliwafungia Newcastle bao la moja.
Huko Ewood Park nyumbani kwa Blackburn Rovers, Matt Derbyshire alifunga goli moja na la ushindi baada ya Roque Santa Cruz kumpasia kwa kichwa safi cha ujanja kufuatia krosi murua ya Carlos Villanueva na hivyo kuwapiga wageni wao Fulham kwa bao 1-0.

No comments:

Powered By Blogger