Friday 19 September 2008

FERGUSON NA WENGER: sasa ni marafiki?

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ilikuwa si kitu cha ajabu kusikia au kuona Mameneja Sir Alex Ferguson wa Manchester United na Arsene Wenger wa Arsenal wakizozona huku timu zao zikipambana vikali uwanjani.
Lakini kwa sasa kuna kila dalili mizozo hiyo imekwisha na Mameneja hao wana msimamo mmoja.
Hali hii ilithibitika siku kadhaa zilizopita walipokuwa wageni rasmi waalikwa kwenye chakula cha usiku cha Chama cha Mameneja wa Ligi huko Uingereza ili kutunisha mfuko wao wa kusaidia jamii.
Katika hafla hiyo, Mameneja wote hao wawili walipata fursa ya kuhutubia na wote walionyesha sasa wana msimamo mmoja. Wote waliwaunga mkono Kevin Keagan aliekuwa Meneja wa Newcastle na Alan Curbishley wa West Ham waliolazimika kujiuzulu kwa sababu ya kuingiliwa kazi zao na wamiliki wa Klabu hizo.
Sir Alex Ferguson alitamka:'Kwa mazingira ya sasa ambayo klabu zinatawaliwa na Wenyeviti vijana matajiri sana, lazima uwe na mafanikio kama Meneja lakini utapataje mafanikio hayo ikiwa Mwenyekiti huyohuyo anawauza Wachezaji wako bora nyuma ya mgongo wako ili azidi kutajirika na vilevile anataka timu ishinde! Bila shaka Keagan na Curbishley wamefanya kitendo cha heshima kujiuzulu ili kutetea msimamo wao!'
Wenger akamuunga mkono Ferguson kwa kusema:'Meneja ni mtu muhimu sana kwenye klabu!! Kama si muhimu kwanini anafukuzwa kazi timu ikifanya vibaya?' Nadhani mimi na Ferguson tuna bahati kwani tuliweza kufanya kazi bila kuingiliwa hivyo tulikuwa huru kujenga timu bora.'
Walipoulizwa kuhusu uhsiano wao binafsi kwa sasa, Wenger alitamka:'Sasa tuna maelewano vizuri sana kati yetu na tunaheshimiana sana.'
Nae Ferguson akaongeza:'Sasa tunakaa na kunywa mvinyo na chakula pamoja! Tushakutana mara nyingi kwenye vikao vya Mameneja hasa kule Geneva. Wote tuna timu changa na bora na tuna ushindani.'

No comments:

Powered By Blogger