Sunday 1 March 2009

Liverpool wazidi kuporomoka, Chelsea wachupa juu yao na Arsenal bado doro!!!

Chelsea walipata goli la ushindi la utata kwenye dakika ya 90 mfungaji akiwa Frank Lampard, goli ambalo Meneja wa Wigan Steve Bruce amelipinga na kudai Mfungaji alimchezea rafu Beki wake Melchiot, na sasa Chelsea wameweza kuwapita Liverpool ambao walifungwa 2-0 na Middlesbrough na hivyo kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa LIGI KUU England.
Chelsea walipata bao lao la kwanza kupitia Nahodha John Terry dakika ya 25 lakini Wigan walisawazisha dakika ya 82 kupitia Olivier Kapo.
Liverpool wakicheza ugenini Riverside nyumbani kwa Middlesbrough timu ambayo mwendo wake hauridhishi walijikuta wakianza kwa balaa pale Mchezaji wao Xabi Alonso alipojifunga mwenyewe kufuatia kona iliyopigwa dakika ya 32.
Tuncay Sanli alipachika bao la pili kwa Middlesbrough dakika ya 63 na kuwafanya Liverpool waporomoke toka nafasi ya pili hadi ya 3 ingawa wako pointi sawa na Chelsea, wote wakiwa na 55, lakini Chelsea ana tofauti ya magoli bora.
Timu hizi sasa zimecheza mechi 27 kila moja huku Manchester United iliyocheza mechi 26 bado inaongoza ikiwa na pointi 62.
Nao Arsenal wameendelea kudorora pale walipotoka suluhu ya 0-0 na Fulham hii ikiwa mechi yao ya nne sasa ya LIGI KUU wakimaliza bila kufunga hata goli moja.
Arsena bado wako nafasi ya 5 wakiwa wamecheza mechi 27 na wana pointi 46. Juu yao wapo Aston Villa waliocheza mechi 26 na wana pointi 51.
.............................Baada ya mechi, NINI WAMESEMA?
Rafael Benitez, Meneja wa Liverpool: 'Nusu saa ya kwanza tulipata nafasi 5 za wazi! Kabla ya mechi hii tulijua kushinda Ligi ni ngumu, sasa ni wazi ni ngumu kabisaaa!!'
Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal: 'Tumeanza kupata wasiwasi! Hili ni pigo kubwa kwetu! Tuna ubutu sasa na ni ngumu kusema tatizo ni nini- ama kisaikolojia, au mbinu au ufundi! Nikiongea zaidi tatizo litakuwa kubwa zaidi!'

No comments:

Powered By Blogger