Thursday, 20 August 2009

Man U mashakani?
Mechi mbili tu ndani ya Msimu mpya wa Ligi zilizochezwa na Mabingwa Manchester United, zote zikiwa dhidi ya Timu zilizopanda Daraja msimu huu, moja waliyoifunga Birmingham 1-0 na ya pili kufungwa na Burnley 1-0, tayari baadhi ya watu wameanza kuchonga kuwa matokeo yote hayo ni sababu ya pengo kubwa la Ronaldo na ufa wa kukosekana kwa Carlos Tevez.
Ingawa katika mechi hizo mbili za kwanza za Ligi Man U wameonekana kupwaya kidogo, kuwa butu na kukosa spidi ya kuponyoka Mabeki, wengi wamesahau ile “desturi” ya Mabingwa hao kuanza Ligi kwa upole na matokeo mabovu lakini mwishowe hupamba moto na hatimaye kuibuka Mabingwa, mtindo uliowafanya wanyakue Ubingwa mara 11 katika Misimu 17 iliyopita ikiwemo kuwa Bingwa kwa Misimu mfululizo mitatu iliyopita.
Wengi pia hawakuona au wanasahau kuwa katika mechi hizo mbili za kwanza Man U imewakosa baadhi ya Vigogo wao ambao ni majeruhi. Listi hii wamo Kipa Edwin van der Sar, Mabeki Rio Ferdinand na Nemanja Vidic, Viungo Owen Hargreaves na Darren Fletcher.
Vilevile, Sir Alex Ferguson, Meneja wa Man U, alibadilisha Wachezaji 6 kutoka kile Kikosi kilichoifunga Birmingham katika mechi na Burnley.
Graeme Souness, Mchezaji na Meneja wa zamani wa Liverpool, anaeleza: “Ni kweli Ronaldo ni Mchezaji Bora Duniani alieibeba Man U kwa misimu miwili iliyopita lakini huweza ukapima pengo lake kwa sasa! Lakini, kama Michael Owen atakuwa fiti kwa muda mrefu atafunga goli nyingi tu! Najua ntaudhi watu wengi nikisema hili lakini ukweli ni kwamba Owen hajawahi kucheza Timu nzuri yenye Wachezaji wazuri kama Manchester United! Atakuwa mashine ya magoli tu!”
Juu ya yote kuna Mdau amedai bahati na hatima ya Timu zote huwa ni mzunguko unaoamuliwa na jinsi Wachezaji Bora wanapoingia au kuhama Timu.
Kitu cha mwisho kabisa alichokifanya Patrick Viera akiwa na Jezi ya Arsenal ni kuifungia Klabu hiyo bao la ushindi katika mikwaju ya penalti tano tano katika Fainali ya Kombe la FA mwaka 2005 na kuibebesha Arsenal Kombe hilo.
Kisha akahama- na tangu wakati huo Arsenal haijashinda Kombe lolote!!!
Alipoondoka David Beckham Old Trafford mwaka 2003, Manchester United hawakuchukua Ubingwa kwa miaka minne!!
Ni kweli Mchezaji Bora Duniani, Cristiano Ronaldo, amehama na haiwezekani kumpata mbadala, na, ingawa Manchester United, kama “desturi” yake imeonyesha kwa mara nyingi tena mwanzo wa kusuasua kwenye Ligi, utakuwa mwehu ukimpinga Sir Alex Ferguson kwani historia itakusuta!!!
Yeye ni gwiji wa kuleta marekebisho na mafanikio!!!

No comments:

Powered By Blogger