Monday, 7 December 2009

LIGI KUU England: Everton 2 Tottenham 2;
Fulham 1 Sunderland 0
Tottenham waliumwaga uongozi wa mabao 2-0 waliokuwa nao hadi dakika ya 78 na kuwaruhusu Everton kusawazisha na kuifanya mechi imalizike 2-2.
Ingawa Everton walisawazisha, Tottenham bado walikuwa na nafasi nzuri ya ushindi kwani walipewa penalti dakika za majeruhi lakini Jermaine Defoe alishindwa kufunga kwani mkwaju wake uliokolewa na Kipa Tim Howard.
Katika mechi hii ya Ligi Kuu iliyochezwa jana nyumbani kwa Everton Goodison Park, mechi ilikuwa 0-0 hadi mapumziko.
Dakika 2 baada ya kipindi cha pili kuanza Jermaine Defoe aliifungia bao Tottenham na Michael Dawson akaongeza bao la pili.
Everton walipata bao la kwanza kupitia Luis Saha dakika ya 78 na Tim Cahill akasawazisha.
Huko Craven Cottage nyumbani kwa Fulham, hapo jana wenyeji Fulham walipata bao moja na la ushindi kupitia Bobby Zamora dakika ya 7 na kuibwaga Sunderland kwenye mechi ya Ligi Kuu.
England yakana Wachezaji kupewa Viagra kwenye Fainali Kombe la Dunia!!!
FA, Chama cha Soka England, kimekana vikali taarifa zilizozagaa kuwa Wachezaji wa Kikosi cha England kwenye Fainali Kombe la Dunia mwakani huko Afrika Kusini watapewa dawa aina ya Viagra ili kumudu kucheza katika viwanja vilivyo juu sana toka usawa wa bahari ambako hewa ya oksijeni huwa pungufu na hivyo kufanya kupumua kuwe shida.
Inaaminika dawa ya Viagra, licha ya kuongeza nguvu za tendo la ndoa, pia humfanya mtu apumue vizuri hasa kwa Wanamichezo wanaoshindana kwenye viwanja vilivyo juu sana ambako kupumua kunakuwa shida.
Ripoti hizo za Wachezaji kupewa Viagra zilisema Kocha wa England Fabio Capello ndie alieamrisha kupewa dawa hizo lakini FA imekana taarifa hizo na kuziita za uzushi huku wakisistiza suala kucheza kwenye viwanja vya mwinuko wa juu linafanyiwa utafiti na Jopo lao la Madaktari ili kupata njia sahihi ya kukabiliana nalo.

No comments:

Powered By Blogger