Friday 27 March 2009

Mama Mzazi na Mama Mkwe wa John Terry waonywa na Polisi kwa 'udokozi' Madukani!!!!!

Familia ya Nahodha wa Chelsea na Timu ya Taifa ya England, John Terry, imekumbwa na fedheha pale Polisi walipothibitisha kuwa Bibi Sue Terry [50], ambae ni Mama Mzazi wa John Terry na Bibi Sue Poole [54], Mama Mkwe wa Mchezaji huyo, wamepewa onyo baada ya kukiri tuhuma za udokozi kwenye Maduka mawili makubwa ya Marks & Spencer na la Tesco yaliyopo Weybridge, Surrey.
Inasemekana John Terry amewanunulia kina Mama hao Nyumba huko Surrey na yeye mwenyewe na Mkewe wanaishi pia maeneo hayo.
Lakini, Mwanasheria wa John Terry amedai kina Mama hao walikubali kosa la udokozi huo huko Polisi kimakosa na yeye sasa yuko kwenye harakati za kusafisha majina yao.

Refa afyatua Kadi Nyekundu 18 katika Mechi moja!!!!!

Huko Argentina, kwenye mechi ya Primera C, yaani mechi ya Timu za Daraja la 3, kati ya wenyeji Barracas Bolivar na wageni General Lamadrid, Refa alitoa Kadi Nyekundu 18 katikati ya kipindi cha pili cha mechi baada ya kutokea fujo na ngumi uwanjani.
Huku wenyeji Barracas Bolivar wakiongoza 3-0, mashabiki wa timu hiyo walikuwa wakiwazomea na kuwakejeli General Lamadrid, ndipo Wachezaji watatu wa Lamadrid na Watu wanne wa benchi la ufundi wakaanza kuzozana na mashabiki hao.
Mzozo huo ukazua ngumi na mapigano makali kati ya Wachezaji wote 11 wa Lamadrid wakisaidiwa na Wachezaji 7 wa akiba.
Fujo hizo zilisimama pale tu Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia walipoingilia na ndipo Refa wa mechi hiyo akawalamba Wachezaji wote 11 wa General Lamadrid Kadi Nyekundu na kuongeza Kadi nyingine Nyekundu 7 kwa Wachezaji wote wa Akiba wa timu hiyo.
Sasa itabidi Klabu ya General Lamadrid ichezeshe Wachezaji wa Akiba na Timu ya Vijana kwenye mechi ifuatayo ya Ligi.

Beckham asema kuvunja rekodi si kusudio lake, kuipeleka England Fainali Kombe la Dunia huko Afrika Kusini 2010 ndio lengo lake!!!!!

David Beckham, ambae yeye na Mchezaji wa zamani Bobby Moore, ndio wanashikilia rekodi ya kuchezea England mechi nyingi kwa kucheza mechi 108 kwa Wachezaji wa mbele [Rekodi ya mechi nyingi inashikiliwa na Kipa Peter Shilton aliechezea mechi 125], amesema yeye anachotaka ni kuiona England Fainali Kombe la Dunia mwaka 2010 huko Afrika Kusini.
Beckham ambae yumo kwenye Kikosi cha England kinachofanya mazoezi kwa mechi ya kirafiki ya Jumamosi dhidi ya Slovakia na ile ya mchujo Kombe la Dunia hapo Jumatano dhidi ya Ukraine atafikisha mechi 109 akicheza Jumamosi na hivyo kumpita Sir Bobby Moore.

No comments:

Powered By Blogger