Thursday, 26 March 2009

Meneja wa England, Fabio Capello, amwita Rooney mwehu!!!

Kwenye kambi ya mazoezi ya Kikosi cha Timu ya England kinachojitayarisha kwa mechi ya kirafiki ya Jumamosi watakapocheza na Slovakia na ile ya mchujo wa Kombe la Dunia dhidi ya Ukraine ya Jumatano, Fabio Capello alimwita kwa mzaha Rooney: 'Kwa nini ulipiga ngumi kibendera cha kona? Wewe ni mwehu, ni mtu mwehu!!'
Capello anadaiwa kusema maneno hayo akimaanisha kitendo cha Rooney alichokifanya mara baada ya kupewa Kadi Nyekundu na Refa Phil Dowd kwenye mechi ambayo Man U ilifungwa 2-0 na Fulham.
Inasemekana vilevile, Capello alifanya mazungumza ya undani na Ashley Cole wa Chelsea na Steven Gerrard wa Liverpool ambao wote walikwaruzana na Polisi huku Cole akipata onyo kwa ulevi na ubishi toka kwa Polisi lakini Gerrard mpaka sasa yuko Mahakamani akikabiliwa na kesi dhidi yake.
Inaelekea nia ya Capello ni kutaka kudumisha nidhamu kwa Wachezaji wake Mastaa tegemezi ili wahakikishe England inafuzu Fainali za Kombe la Dunia 2010 huko Afrika Kusini.
England mpaka sasa ni kinara kwenye Kundi lake la mchujo akiwa juu ya Croatia, Ukraine, Belarus, Kazakhstan na Andorra akiwa na pointi 12 kwa mechi nne huku Croatia na Ukraine ambao wamefungana nafasi ya pili wana pointi 7.

Marefa England wataka ufafanuzi kwanini Kadi zao Nyekundu zinafutwa na FA!!!

Bodi ya Marefa wa Kulipwa wa England (PGMO) kimeitaka FA England itoe ufafanuzi ni sababu gani na vipengele vipi vimeifanya kufuta baadhi ya Kadi Nyekundu zinazotolewa kwenye mechi za LIGI KUU England.
Hivi juzi Kadi Nyekundu walizotwangwa Kipa Brad Friedel wa Aston Villa na Mlinzi wa Sunderland George McCartney zilifutwa na FA baada ya rufaa ya klabu zao.

Man U kucheza AUDI CUP huko Ujerumani!!

Mabingwa wa England, Ulaya na Dunia, Manchester United, wamealikwa na Kampuni ya Magari aina ya Audi ya Ujerumani kucheza kwenye Kombe lao majira ya joto yajayo na wataungana na Klabu machachari ya zamani ya Diego Maradona, Boca Juniors ya Argentina, AC Milan ya Italy na Bayern Munich ya Ujerumani.
Man U watapambana na Boca Juniors tarehe 29 Julai 2009 na siku hiyo hiyo Bayern Munich itaikwaa AC Milan.
Washindi wa mechi hizo watacheza Fainali tarehe 30 Julai 2009 huku mechi hiyo ikitanguliwa na waliofungwa mechi za utangulizi ili kupata Mshindi wa Tatu.

No comments:

Powered By Blogger