Sunday 22 November 2009

Bolton 0 Blackburn 2
Bolton leo wamepata kipigo cha 2-0 wakiwa nyumbani kwao toka kwa Blackburn ambao hawajahi kushinda mechi ya Ligi Kuu wakiwa ugenini katika mechi 10 za mwisho za ugenini walizocheza mpaka hii leo.
Blackburn leo wamecheza mechi hii bila ya Meneja wao Sam Allardyce ambae ni mgonjwa anaetegemewa kufanyiwa operesheni ya moyo wiki hii.
Nafasi yake ilichukuliwa na Meneja Msaidizi Neil McDonald.
Bao la kwanza lilifungwa na David Dunn kwa shuti kali akiwa nje ya boksi kwenye dakika ya 30 kipindi cha kwanza.
Dakika ya 74, Blackburn wakapata bao la pili ambalo Bolton walijifunga wenyewe na jinsi lilivyofungwa ilikuwa kama Ze Komedi!
Brett Emerton wa Blackburn akiwa winga ya kulia alipiga krosi ambayo kwa wengi ilikuwa ni ya kubahatisha lakini Kipa wa Bolton Jussi Jaaskelainen akatoka golini kuifuata bila Sentahafu wake Sam Ricketts kujua na Ricketts akairukia krosi hiyo na kupiga kichwa kuelekea golini kumrudishia Kipa akidhani Kipa Jaaskelainen yupo kumbe ni goli tupu na kujifunga mwenyewe!
Wenger: “Tunazungumza na Gallas, Rosicky na Vela kuwaongezea mkataba”
Arsene Wenger ametangaza kuwa wako kwenye mazungumzo na Wachezaji wake William Gallas, Tomas Rosicky na Carlos Vela ili waongezewe na kupewa mikataba mipya.
Gallas na Rosicky wako kwenye mwaka wa mwisho wa mikataba yao inayoisha mwishoni mwa msimu huu na kisheria ifikapo Januari watakuwa huru kuongea na Klabu nyingine yeyote ili kuhamia Klabu hizo.
Lakini Meneja wa Arsenal Wenger anaamini Wachezaji hao watabaki Arsenal.
Kuhusu Vela, Wenger amesema: “Hatujapata ofa yeyote kuhusu Vela na sisi tunataka kuuboresha mkataba wake. Ni Mchezaji mdogo lakini mbele yake kuna Vijana wazuri kama yeye. Alipoondoka Adebayor sikuhangaika kupata mbadala wake kwani najua Vela yupo na ni mzuri!”
Fergie: “Ni ngumu kununua Mchezaji Januari!”
Bosi wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesema hadhani kama atanunua Mchezaji wakati dirisha la uhamisho litakapofunguliwa mwezi Januari ingawa amehusishwa na Wachezaji kadhaa akiwepo Kijana mzuri sana wa Everton Jack Rodwell.
Lakini Ferguson amekataa na kusisitiza hawezi kulipa dau la bei mbaya kwa Mchezaji yeyote na vile vile hana tatizo na Kikosi chake cha sasa.
Ferguson amesema: “Kuna Wachezaji wengi kwenye soko lakini Klabu zao zinawathamini kwa dau la Pauni Milioni 50! Kwa bei hiyo sioni kama Wachezaji hao wana thamani hiyo!”

No comments:

Powered By Blogger