Tuesday 24 November 2009

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: Leo Liverpool wanaombea maajabu!!! Arsenal wanahitaji pointi moja tu kusonga mbele!!
Liverpool wako ugenini huko Hungary kupambana na Debrecen na ili wabaki na matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE ni lazima washinde na pia waombe Mungu Fiorentina wasiifunge Lyon katika mechi zinazochezwa leo za KUNDI E.
Katika KUNDI H, Arsenal leo wako nyumbani Emirates Stadium kucheza na Timu ya Ubelgiji Standard Lege na Arsenal, wakiwa wamebakisha mechi 2 katika Kundi lao, wanahitaji pointi moja tu katika hizo mechi 2 ili kusonga Raundi ya Pili ya Mtoano.
Mechi nyingine kwenye Kundi la Arsenal ni kati ya Olympiakos na AZ Alkmaar.
Refa Alan Wiley hamshitaki Fergie!
Refa Alan Wiley amesema kuwa hana nia ya kumshitaki Sir Alex Ferguson Mahakamani ili kudai fidia kwa kauli ya kashfa aliyoitoa Meneja huyo wa Manchester United alipodai Refa huyo hayuko fiti kuchezesha mechi.
Ferguson alitoa kauli hiyo Oktoba 3 mara baada ya Man U kutoka sare 2-2 na Sunderland katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Old Trafford.
Wiley amethibitisha hataki kuendeleza ugomvi na Ferguson licha ya Allan Leighton, Katibu wa Chama che Kutetea Maslahi Marefa, kutoa shinikizo Ferguson adaiwe fidia Mahakamani.
Ferguson alimwomba msamaha Refa Wiley na pia kukiri makosa yake kwa FA waliomshitaki na kisha kumwadhibu kufungiwa mechi 2 huku mechi 2 nyingine zikiwekwa kiporo ili kuchunga mwenendo wake hadi msimu wa 2010/11 utakapoisha na pia alipigwa faini ya Pauni 20,000.
Wachezaji Wigan kurudisha viingilio vya Mashabiki wao walioshuhudia kipigo chao cha mabao 9!!!!!
Mashabiki 400 wa Wigan waliosafiri hadi Jijini London Uwanjani White Hart Lane na kushuhudia Timu yao ikifumuliwa mabao 9-1 na Tottenham kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Jumamosi watarudishiwa pesa walizolipa kiingilio na watakaolipa pesa hizo ni Wachezaji wenyewe wa Wigan.
Kipigo hicho cha Wigan cha 9-1 ni kikubwa cha pili kwenye historia ya Ligi Kuu cha kwanza kikiwa kile cha mwaka 1995 wakati Manchester United walipowashushia Ipswich Town kipigo cha mabao 9-0.
Nahodha wa Wigan, Mario Melchiott, amesema wao wamehuzunika na ili kuomba msamaha kwa Mashabiki wao, wameamua wao wenyewe kutoa pesa zao wenyewe kuwarudishia Mashabiki wao walioshuhudia kipigo hicho.
FIFA yaitisha kikao cha dharura Desemba!!!
FIFA imeitisha kikao cha dharura mwezi ujao ili kujadili matukio yaliyotokea kwenye mechi za Mtoano kutafuta Timu za mwisho zilizoingia Fainali Kombe la Dunia.
Tukio kubwa lililoitikisa Dunia ya Soka ni pale Ufaransa walipotinga Fainali za Kombe la Dunia kwa msaada wa ‘upofu’ wa Refa Martin Hansson wa Sweden ambae hakumwona Thierry Henry akishika mpira na kumpasia William Gallas katika dakika ya 104 ya dakika za nyongeza na Gallas kuisawazishia Ufaransa na kufanya matokeo kuwa 1-1 dhidi ya Ireland na hivyo kuingia Fainali.
Licha ya Henry kukiri maovu yake na Ireland kudai mechi irudiwe, FIFA iling’ang’ana ‘uamuzi wa Refa ni wa mwisho’.
Matukio mengine ni yale yaliohusu mechi za Misri na Algeria ambazo zilibidi zirudiane uwanja nyutro huko Khartoum, Sudan baada ya kulingana kila kitu na ambako, hatimaye, Algeria alishinda 1-0 na kuingia Fainali Kombe la Dunia.
Kabla ya mechi ya awali iliyochezwa huko Cairo, Misri basi la Wachezaji wa Algeria lilipigwa mawe na Wachezaji kadhaa wakajeruhiwa. Kitendo hicho kiliibua hasira huko Nchini Algeria ambako Raia kadhaa wa Misri waishio huko waliumizwa, mali zao kuharibiwa na wengine walilazimika kuikimbia Nchi hiyo.
Vilevile, mechi kadhaa za Kombe la Dunia zilikuwa zimegubikwa na maamuzi ya utata wa Marefa.
Pia, FIFA imekisimamisha Chama cha Soka cha Iraq baada ya Chama hicho kuingiliwa na Serikali ya Iraq katika uendeshwaji wake.
Kikao hicho kinategemewa kufanyika wiki ijayo huko Cape Town, Afrika Kusini ambako pia kutapangwa Makundi na Ratiba ya Fainali za Kombe la Dunia.

No comments:

Powered By Blogger