Monday, 23 November 2009

Licha ya kusuasua, Benitez aota kumaliza Ligi wakiwa juu!!!
Bosi wa Liverpool Rafael Benitez amesisitiza Timu yake itamaliza Ligi Kuu England ikiwa kwenye 4 bora na hivyo kucheza Ulaya licha ya juzi kutoka sare 2-2 na Manchester City kwenye mechi ya Ligi Kuu, hiyo ikimaanisha katika mechi 13 za Ligi Kuu walizocheza msimu huu wameshinda 6, suluhu 2 na kufungwa mechi 5 na wako pointi 13 nyuma ya vinara Chelsea huku wakiwa nafasi ya 7.
Ndoto ya Benitez imekuja huku akijipa matumaini kuwa Kikosi chake kina majeruhi kadhaa na wakipona basi wataonyesha makali yao.
Benitez ametamka: “Wachezaji wetu wote wakirudi tutaanza kushinda!”
Huenda FIFA ikamwadhibu Henry!!!
Kuna taarifa kuwa Kamisheni ya Nidhamu ya FIFA inachunguza tukio la Thierry Henry kuushika mpira na kumpasia mwenzake William Gallas aliefunga bao na kufanya mechi ya Ufaransa na Republic of Ireland iwe 1-1 na hivyo kuipa Ufaransa ushindi wa kuingia Fainali Kombe la Dunia.
Kitendo hicho hakikuonekana na Refa Martin Hansson.
Licha ya Thierry Henry mwenyewe kuungama makosa yake na madai ya Ireland na Wadau wengine kutaka mechi hiyo irudiwe, FIFA imeng’ang’ania msimamo wake wa kihistoria kuwa ‘uamuzi wa Refa ni wa mwisho’ na hivyo hamna uwezekano mechi hiyo kurudiwa.
Taarifa hizo zimesema ndani ya wiki mbili zijazo Kamisheni hiyo itakutana na kutoa uamuzi kama Henry anastahili adhabu kwa ‘kitendo kisicho cha uanamichezo’.
Taarifa hizo zimetoa mifano ya FIFA kuwachukulia hatua Wachezaji hapo nyuma kwa makosa ambayo Refa hakuyaona na ametajwa Mchezaji Marco Materazzi wa Italia aliefungiwa mechi 2 na kupigwa faini Pauni 4,500 kwa kumchokoza Mfaransa Zinedine Zidane katika Fainali ya Kombe la Dunia na kumsababisha Zidane akasirike na kumtwanga kichwa Materazzi na hivyo Zidane kupewa Kadi Nyekundu na Refa huku Materazzi hakupewa Kadi yeyote.
Wakati huohuo Refa aliehusika na mzozo wa Thierry Henry kuushika mpira, Martin Hansson kutoka Sweden ambae hakuona kitendo hicho, huenda asipate msukosuko wowote toka FIFA kwani yumo kwenye listi ya awali ya Marefa watakaochezesha Fainali Kombe la Dunia.
Timu ya Beckham LA Galaxy yaukosa Ubingwa Marekani!!
Los Angeles Galaxy leo alfajiri imefungwa kwa penalti kwenye Fainali ya Ubingwa wa Marekani, MLS, na Real Salt Lake ambao wameutwaa Ubingwa wa Marekani.
Timu hizo zilitoka sare 1-1 na ndipo kwenye penalti LA Galaxy wakatolewa 5-4.
Mechi hiyo ilichezwa Mjini Seattle huko Marekani.
Ferguson: “England hawawezi kuchukua Kombe la Dunia!”
Licha ya uwezekano wa Wachezaji wake 9 kuwemo kwenye Kikosi cha England kitakachocheza Fainali za Kombe la Dunia huko Afrika Kusini mwakani, Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson ametamka haamini kama England watashinda na anaiona Brazil kama ndio watakaobeba Kombe hilo.
Ferguson amenena: “Sioni mtu atakaepita kwa Brazil! Wao ni kama mtambo wa Wachezaji bora! Msimu uliokwisha kwenye UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Brazil walitoa Wachezaji 103 na ni 13 tu walitoka England!”
Wachezaji wa Manchester United ambao wamo kwenye uwezekano wa kuwa kwenye Kikosi hicho cha Kombe la Dunia ni Wayne Rooney, Rio Ferdinand, Michael Carrick, Wes Brown, Ben Foster, Owen Hargreaves, Michael Owen, Gary Neville na Danny Welbeck.

No comments:

Powered By Blogger