Monday 6 April 2009

Dunia nzima inajiuliza Federico Macheda, kijana mdogo shujaa mpya wa Man U , ni nani?
Mwenyewe asema: 'Ni ndoto!!'

Kijana wa miaka 17 mzaliwa wa Rome, Italia, Federico Macheda, ambae huchezea Timu ya Akiba ya Man U na jana ikiwa ni mara ya kwanza kabisa kuchezea Kikosi cha kwanza, alijiandikia historia kwa kuifungia Man U bao la ushindi dhidi ya Aston Villa katika dakika za majeruhi na kuwarusha Mabingwa hao hadi kileleni mwa LIGI KUU England.
Leo dunia nzima ya soka inajiuliza: Macheda ni nani na katokea wapi?
Mwenyewe Federico Macheda anaelezea: 'Nilikuwa nikiiota siku kama hii!! Niligeuka na kupiga shuti kisha nikashangilia na kuikimbilia familia yangu!!'
Macheda alienda kwa Watazamaji kumkumbatia Baba yake Mzazi aliekuwa akibubujikwa na machozi ya furaha.
Kitendo hicho kilifanya Macheda apewe Kadi ya Njano na Refa Mike Riley.
Meneja wake, Sir Alex Ferguson, alisema: 'Nilimpa hongera! Nikamwambia asivimbe kichwa ila aongeze juhudi. Kuchezesha kikosi kile na chipukizi wale ni kucheza bahati nasibu! Ni hatari lakini ni lazima ujaribu bahati wakati mwingine! Hatukujihami vizuri lakini siku zote tunajiamini tuna uwezo wa kufunga magoli!'
Baada ya mechi hiyo na Aston Villa ambayo mbali ya kuwa shujaa wa Man U, Wadhamini rasmi wa LIGI KUU England, Kampuni ya Barclays, walimteua kuwa ndie MCHEZAJI BORA WA MECHI.
Je ni nani Macheda?
Huko Old Trafford huitwa 'Kiko' ikiwa ndio a.k.a yake.
Macheda alizaliwa Rome mwaka 1991 na kuanza soka lake akiwa na Timu ya Watoto ya Klabu ya Lazio ya Italia na angeendelea kubaki hapo lakini sheria za Italia haziruhusu kumsaini mtu aliye chini ya miaka 18 kuwa Mchezaji wa Kulipwa na ndipo Man U wakamnyakua toka Lazio mwaka 2007 akiwa na miaka 16 na kumsainisha mkataba wa kuwa mwanafunzi kwenye Chuo chao cha Soka.
Aliposaini mkataba huo Familia yake , yaani Baba, Mama na mdogo wake, wote wakahamia Manchester.
Mwaka jana, mwezi Agosti, alipotimiza miaka 17, akasaini mkataba wa kuwa Mchezaji wa Kulipwa wa Man U.
Macheda akiwa kwenye Kikosi cha Timu ya Akiba kilicho chini ya usimamizi wa Nyota wa zamani Ole Gunnar Solskjaer ameshafunga goli nane kwenye mechi nane alizocheza yakiwemo magoli matatu kwenye mechi dhidi ya Timu ya Akiba ya Newcastle mwezi uliopita.
Kijana huyo kwa sasa yuko kwenye Kikosi rasmi cha Wachezaji 25 kilichosajiliwa UEFA kwa mashindano ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE.
Macheda pia yumo kwenye Timu ya Taifa ya Italia ya Vijana wa chini ya umri wa miaka 18.

No comments:

Powered By Blogger