Saturday 4 April 2009

Ligi Kuu leo: Shearer kuanza kibarua, Berbatov majeruhi, Fabregas uwanjani, Zaki matatani!!!

Baada ya kutochezwa kwa wiki mbili sasa ili kupisha mechi za Timu za Taifa kwenye michujo ya Kombe la Dunia, leo LIGI KUU England inarudi dimbani huku Newcastle, watakaocheza na Chelsea, wakiwa na Meneja mpya aliekuwa Mchezaji wao wa zamani, Alan Shearer, ambae amesimikwa hapo kwa kazi moja tu na nayo ni kuinusuru Newcastle isporomoke daraja.
Kwa sasa Newcastle iko nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi ikiwa ni nafasi ya 3 toka mkiani na kawaida timu za mkiani, yaani nafasi ya 18, 19 na 20, hushushwa daraja.
Ingawa Newcastle wako nyumbani leo, uwanjani kwao St James Park, kazi yao ni ngumu sana kwani wanakumbana na Timu ngumu ya Chelsea iliyo nafasi ya 3 na ambayo bado ina matumaini makubwa ya kuwa Bingwa.
Nao Mabingwa wa LIGI KUU, Maanchester United, kesho watakuwa kwao Old Trafford huku wakiwa wamekumbwa na balaa la kuwakosa Wachezaji wao wakubwa kwenye mechi dhidi ya Aston Villa.
Wayne Rooney na Nemanja Vidic wamefungiwa kwa kuwa na Kadi Nyekundu na Berbatov ni majeruhi kwa kuumia enka.
Hivyo mbele watamtegemea Tevez tu ambae hali yake haijathibitishwa kwani aliwasili jana jioni akitokea Marekani Kusini alikokuwa na Timu yake ya Taifa ya Argentina.
Huko Wigan nako mambo si shwari kwani baada ya Mmisri Mido kumshutumu Mmisri mwenzake, Amr Zaki, wote wakiwa Wachezaji wa Wigan, Meneja wa Wigan Steve Bruce ametangaza kuwa watamchukulia hatua kali sana Zaki kwa kuchelewa kurudi kutoka Misri alikochezea Timu ya Taifa ya Misri iliyocheza kwenye dro ya 1-1 na Zambia kwenye mechi ya Kombe la Dunia.
Steve Bruce amesema hii ni mara ya nne kwa Zaki kuchelewa kurudi na kila mara amekuwa akipigwa faini lakini safari hii watampa adhabu kali sana.
Kesho Wigan ni wageni wa Everton.
Arsenal leo wanawakaribisha Manchester City Emirates Stadium na vilevile watamkaribisha Nahodha wao Cesc Fabregas aliekuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu baada ya kuumia.
Vilevile, Wachezaji wengine wa Arsenal walioumia na sasa kupona na leo watakuwa kikosini ni pamoja na Emmanuel Adebayor, Theo Walcott na Nicklas Bendtner.
Lakini Robin van Perise, Eduardo, Abou Diaby na Samir Nasri wote watakuwa nje kwa kuwa majeruhi.

No comments:

Powered By Blogger