Saturday 5 July 2008


RONALDO KUPASULIWA!
Cristiano Ronaldo anategemewa kufanyiwa operesheni ya kisigino wiki ijayo na hii inamaanisha atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita kuanzia hapo na hivyo kuukosa mwanzo wa msimu mpya wa LIGI KUU UINGEREZA ambao utaanuliwa rasmi tarehe 10 Agosti 2008 kwa pambano la kugombea NGAO YA HISANI kati ya Bingwa wa LIGI KUU, Manchester United, na Bingwa wa Kombe la FA, Portsmouth kwenye Uwanja wa Wembley.
LIGI KUU yenyewe inaanza rasmi tarehe 16 Agosti 2008 kwa Man United kupambana na Newcastle.
Kwa sasa Ronaldo yuko kwenye likizo na hatakuwa na timu yake kwenye ziara ya Afrika ambako Man United itatembelea Afrika Kusini na Nigeria mwishoni mwa Julai.
Siku za hivi karibuni utata mkubwa umekuwa ukimzunguka Ronaldo kuhusu hatma yake ambako amehusishwa kuhamia Real Madrid na hata ikabidi Man United waripoti mbinu za Real Madrid kumrubuni Ronaldo kwa FIFA na klabu hiyo itoe kauli kali ‘hauzwi’.
Jana tena Man United wamesisitiza msimamo kuwa hauzwi na kuziita tarifa kuwa anahama ni UPUMBAVU na VICHEKESHO VITUPU.
Hata dada yake Ronaldo amethibitisha Ronaldo hana mpango wa kuhama Man United.
+++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
ADEBAYOR KWENDA BARCELONA?
Wakati Ronaldo bado ni fumbo kuna taarifa za chinichini ambazo zimepewa uzito mkubwa kuwa Klabu ya Barcelona ishakubaliana na Arsenal kumnunua Adebayor kwa Pauni Milioni 30.
Mchezaji huyu alinunuliwa na Arsenal kwa Pauni milioni 5 hivi miaka miwili nyuma toka Klabu ya Monaco na msimu uliopita aliifungia Arsenal mabao 30.
Arsenal inasemekana wamekubali shingo upande kumuuza hasa kufuatia ukweli kwamba mchezaji mwenyewe anataka kuhama kwa sababu tu hamna njia yeyote mshahara wake wa Pauni 35,000 kwa wiki unaweza kupandishwa kwani Klabu ya Arsenal ina kanuni kwamba mishahara ya wachezaji ina viwango maalum huku wengi wakiwa kwenye daraja la Pauni 50,000 kwa wiki.
Inategemewa Adebayor akiwa Barcelona atapata mshahara wa zaidi ya Pauni 100,000 kwa wiki.


No comments:

Powered By Blogger