Friday 30 January 2009

FAINALI YA UEFA CHAMPIONS LEAGUE 2011 KUFANYIKA WEMBLEY

UEFA imeteua Uwanja wa Wembley, uliopo London huko England, kuchezewa Fainali ya Klabu Bingwa Ulaya maarufu kama UEFA CHAMPIONS LEAGUE ya mwaka 2011.
Mara ya mwisho kwa Wembley kuchezewa Fainali kama hiyo ilikuwa mwaka 1992 Barcelona ilipoifunga Sampdoria.
Na mara ya mwisho kwa UEFA CHAMPIONS LEAGUE kuchezewa England ilikuwa 2003 wakati Fainali ilipochezwa Old Trafford nyumbani kwa Manchester United.
Uteuzi wa Wembley unafuatia mchuano mkali na Viwanja vingine viwili vilivyokuwa vinataka fursa hiyo na navyo ni kile cha Munich kiitwacho Allianz Arena na kile cha Berlin kiitwacho Olympiastadion.
Hii itakuwa ni mara ya 6 kwa Wembley kuwa mwenyeji wa Fainali za Klabu Bingwa Ulaya nyingine zikiwa ni kama ifuatavyo pamoja na Timu zilizocheza Fainali hizo:
-1992 Barcelona v Sampdoria 1-0
-1978 Liverpool v Club Brugge 1-0
-1971 Ajax v Panathinaikos 2-0
-1968 Man U v Benfica 4-1
-1963 AC Milan v Benfica 2-1
Fainali ya mwaka huu itachezwa mjini Rome kwenye Uwanja uitwao Stadio Olimpico ambao kwa pamoja hutumiwa na Klabu za Serie A huko Italia za AS Roma na Lazio.
Fainali ya mwakani 2010 itchezewa nyumbani kwa Real Madrid Uwanja wa Santiago Bernabeau huko Madrid, Spain.

LIGI KUU: Uhamisho

Zikiwa zimebaki siku mbili ili dirisha la Uhamisho lifungwe hapo tarehe 1 Februari 2009, harakati za kupata Wachezaji dakika za mwisho zimepamba moto huku tetesi zikizagaa kila kona.
Zilizoshika hatamu ni:

Nahodha wa Bolton Nolan kwenda Newcastle

Kevin Nolan [26] ambae ni Nahodha wa Bolton yuko mbioni kukaguliwa afya ili asaini mkataba kuichezea Newcastle.
Habari hizi zimethibitishwa na Garry Megson Meneja wa Bolton.
Nolan amechezea mechi 323 Bolton tangu alipoanza mwaka 1999.

Diouf kutua Blackburn!

Mchezaji machachari wa Senegal, El-Hadji Diouf [28], yuko mbioni kujumuika tena na aliekuwa Meneja wake wa zamani pale walipokuwa wote Bolton, Sam Allardyce, safari hii wakiwa Klabu ya Blackburn, baada ya kufuzu ukaguzi wa afya.
Diouf kwa sasa ni Mchezaji wa Sunderland.

Blackburn wagomea dau la Pauni Milioni 18.5 la Man City kumnunua Santa Cruz!!

Meneja wa Man City, Mark Hughes, amethibitisha kuwa Blackburn wamegoma kumuuza Mshambuliaji wao nyota toka Paraguay Roque Santa Cruz kwa ofa waliyotoa ya Pauni Milioni 18.5 kwa kuwa Blackburn wanataka Pauni Milioni 20.

Kipa Shay Given wa Newcastle aomba rasmi ahamie Man City

Golikipa wa siku nyingi Newcastle, Shay Givens [32], amewasilisha rasmi klabuni kwake ombi la kutaka kuhama ili kuharakisha uhamisho wake kwenda Manchester City ambao umekwama kufuatia mvutano wa dau la uhamisho.
Newcastle wanataka walipwe Pauni Milioni 8 wakati Man City wako tayari kulipa Pauni Milioni 5 kwa Kipa huyo namba moja wa Newcastle kwa miaka 12 sasa.

No comments:

Powered By Blogger