Monday 27 April 2009

KWA UFUPI:::::::::::::::::

LEO FAINALI YA ALAN SHEARER!!


Newcastle United, ikiwa chini ya Nyota wa zamani Alan Shearer kama Meneja wao, leo usiku wanajitupa uwanjani kwao St James Park kupambana na Portsmouth katika vita yao ya kujinusuru wasishuke Daraja. Newcastle wako nafasi ya 19 kwenye msimamo wa LIGI KUU England ikiwa ni nafasi moja tu toka mkiani na wana pointi 30. Juu yao, kwenye nafasi ya 18, wako Middlesbrough wenye pointi 31 na nafasi ya 17 wako Hull City wenye pointi 34. Nafasi ya 20 na ya mwisho inashikiliwa na West Bromwich wenye pointi 28.
Timu tatu za mwisho, yaani zitazomaliza ligi zikiwa nafasi ya 18, 19 na 20 kwenye ligi , hushushwa Daraja.
Portsmouth wako nafasi ya 14 wakiwa na pointi 37 na ingawa wako afueni kidogo lakini bado hawajasalimika kwani kuna mechi 4 au 5 kwa baadhi ya Timu kumaliza ligi.
Rafael aongeza mkataba Old Trafford hadi 2013!!!!

Chipukizi kutoka Brazil, Rafael da Silva, ameongeza mkataba wake na Manchester United hadi Juni 2013.
Rafael yuko Man U pamoja na pacha mwenzake Fabio, wote wakiwa na miaka 18 tu lakini Rafael ndie alieichukua Manchester United kwa kishindo kwani tangu aanze kuchezea Timu ya kwanza Agosti mwaka jana katika mechi na Newcastle amekuwa na mafanikio makubwa na mpaka sasa ameshacheza mechi 24.
Rafael, anaecheza kama beki wa pembeni kulia, ana nafasi kubwa ya kujenga zaidi jina lake hasa kutokana na kuumia kwa Mabeki wanaomudu nafasi hiyo Nahodha Gary Neville na Wes Brown.
Mtoto wa Sir Alex Ferguson aipandisha timu yake Daraja!!!
Darren Ferguson, mtoto wa Sir Alex Ferguson wa Manchester United, ambae ni Meneja wa Timu ya Peterborough iliyokuwa ikicheza Ligi iitwayo LEAGUE 1 ambalo ni Daraja chini ya COCA COLA CHAMPIONSHIP, Daraja ambalo liko chini ya LIGI KUU England, ameweza kuipandisha Timu hiyo na sasa inaungana na Bingwa wa Ligi hiyo Leicester City kuingia COCA COLA CHAMPIONSHIP msimu ujao.
Peterborough imeshika nafasi ya pili kwenye LEAGUE 1 baada ya kuifunga Colchester bao 1-0.
Klinsman atimuliwa Umeneja Bayern Munich
Staa wa zamani wa Ujerumani, Jurgen Klinsman ambae alikuwa Meneja wa Klabu kongwe ya Bundesliga huko Ujerumani, Bayern Munich, amefukuzwa kazi miezi minane tu tangu ateuliwa baada ya matokeo mabaya ya Timu hiyo.
Juzi, kwenye mechi ya Bundesliga, Bayern Munich ilichapwa bao 1-0 na Schalke matokeo yaliyoifanya Bayern iwe nafasi ya 3 kwenye Ligi na hivyo kuwa hatarini kukosa UEFA CHAMPIONS LEAGUE msimu ujao.
Majuzi tu, kwenye Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Bayern ilibamizwa mabao 5-1 na Barcelona na kutupwa nje ya mashindano hayo.

No comments:

Powered By Blogger