Tuesday 28 April 2009

NUSU FAINALI UBINGWA WA ULAYA: ULAYA MOTO KUWAKA!!! Barcelona v Chelsea leo, kesho Man U v Arsenal!!

UEFA CHAMPIONS LEAGUE leo inaingia hatua ya Nusu Fainali huku England ikitawala Ulaya kwa kuwa na Timu 3 kati ya 4 zilizo Nusu Fainali na leo Barcelona, ndani ya nyumba yao Nou Camp, wanawakaribisha Chelsea. Kesho, ndani ya Old Trafford nyumbani kwa Mabingwa Watetezi wa Kombe hilo, Manchester United, Arsenal atakuwa mgeni wa Bingwa huyo.
Marudiano ya Nusu Fainali hizi ni wiki ijayo wakati Jumanne ijayo Arsenal atakuwa mwenyeji wa Man U na Chelsea atamkaribisha Barcelona ndani ya Stamford Bridge.
Washindi wa Nusu Fainali hizi watapambana kwenye Fainali mjini Rome, Italia mnamo tarehe 27 Mei 2009.
Ndani ya Nou Camp, ngome thabiti ya Barcelona inayoongozwa na Meneja wao Pep Guardiola aliekuwa Mchezaji wa zamani wa Barcelona, Chelsea watakuwa na kazi ngumu sana ya kusimamisha Washambuliaji hatari wa Barcelona kina Lionel Messi, Samuel Eto'o na Thierry Henry wanaolishwa na viungo Andres Iniesta na Xavi.
Kazi ya Chelsea itakuwa ngumu kweli hasa kwani itawakosa Mabeki wao wawilli wa kutumainiwa ambao ni Ricardo Carvalho, alie majeruhi, na Ashley Cole, mwenye Kadi. Nafasi zao zinategemewa kuchukuliwa na Alex na Jose Bosingwa ambae itabidi achezeshwe kama Beki wa kushoto kuziba pengo la Ashley Cole.
Pep Guardiola, Meneja wa Barcelona, anakiri Chelsea wana mibavu kupita wao kwa kusema: 'Niliwaona wakiwatoa Liverpool Robo Fainali. Ni wazuri na wana nguvu sana kupita sisi hivyo ni muhimu sana kwetu kumiliki na kudhibiti mpira na kushinda Nou Camp.'
Guus Hiddink, Meneja wa Chelsea, anasema: 'Messi ni hatari. Lakini ukitaka kumkaba Messi peke yake ni kosa kwani wapo Eto'o na Henry ambao ni hatari kubwa pia!'
NEWCASTLE NA BALAA LA KUSHUKA DARAJA!! SHEARER: 'MUDA UNAYOYOMA!!!'
Newcastle 0 Portsmouth 0
Shujaa wa zamani wa Newcastle kama Mchezaji, Alan Shearer, alieletwa tena Newcastle kama Meneja ili kuinusuru timu toka balaa la kushuka Daraja, jana baada ya suluhu ya 0-0 na Portsmouth nyumbani St James Park, amekiri muda unayoyoma kwa Newcastle kujikwamua na sasa wamebakiwa na mechi 4 tu huku wakiwa wamekwama kwenye eneo la timu 3 zitakazoshushwa daraja.
Timu za Newcastle [nafasi ya 18 pointi 31], Middlesbrough [nafasi ya 19 pointi 31] na West Bromwich [nafasi ya 20 (na ya mwisho) pointi 28] ndizo zipo kwenye nafasi ya Timu 3 zinazoshushwa.
Juu yao, zipo Hull City, nafasi ya 17 pointi 34, Sunderland, nafasi ya 16 pointi 35 na Blackburn, nafasi ya 15, pointi 37.
Mechi inayofuata kwa Newcastle ni safari ya kwenda Anfield nyumbani kwa Liverpool wikiendi hii.
Jermaine Jenas atakiwa atoe maelezo na FA kuhusu madai Refa kawabeba Man U!!!
Baada ya kipigo cha mabao 5-2 na Manchester United, Kiungo wa Tottenham Hotspurs, Jermaine Jenas, ametakiwa atoe maelezo na FA, Chama cha Soka England, ndani ya siku 7 juu ya kauli yake kwamba Refa wa mechi hiyo, Howard Webb, alizidiwa na presha ya kuchezesha mechi Old Trafford nyumbani kwa Man U.
Jenas alikaririwa akisema: 'Refa hata hakufikiria na hata hakusita kutoa penalti!!! Ilikuwa kama vile kisha amua kikianza kipindi cha pili basi atatoa kitu!!'
Katika mechi hiyo, Tottenham walikuwa mbele kwa mabao 2-0 hadi mapumziko lakini kipindi cha pili Man U wakaibuka na kuwanyuka mabao matano na hivyo kushinda 5-2.
Jenas alikuwa akizungumzia bao la kwanza ambalo Refa Howard Webb alitoa penalti baada ya Michael Carrick wa Man U kuangushwa na Kipa Gomes wa Tottenham.

No comments:

Powered By Blogger