Sunday, 12 April 2009

LIGI KUU England yaingia patamu!!!

Man U aongoza kwa pointi 1 mechi 7 mkononi, Liverpool, Chelsea wamfukuza wakiwa na mechi 6 bado!!!

Arsenal ndio mwenye 'Trufu' ya nani Bingwa!!!!!

Vita ya msituni kati ya Ferguson na Benitez yapamba moto!!!!

Mabingwa Watetezi, Manchester United, dhahiri wakionyesha kuyumba ambako kumestaajabisha wadau wengi hasa walipopigwa mechi mbili mfululizo ile na Liverpool na ile na Fulham na kupata ushindi mwembamba mechi mbili zilizofuata baada ya kifaa chao kipya Chipukizi Macheda aka Kiko kuwapa ushindi katika mechi hizo dhidi ya Aston Villa na Sunderland, bado wanang'ng'ania uongozi kwa pointi moja tu ingawa wamecheza mechi moja pungufu.
Nyuma ya Man U wako Liverpool wakifuatiwa karibu na Chelsea huku Arsenal hawako mbali sana.
Zikiwa zimesalia mechi 7 kwa Man U wenye pointi 71, mechi 6 kwa Liverpool wenye pointi 70, mechi 6 kwa Chelsea wakiwa na pointi 67 na Arsenal wana pointi 67 huku nao wamebakiza mechi 6, hakika LIGI KUU England baada ya kutupa uhondo, mashamsham, furaha, karaha, matumaini na kutuumiza mioyo pia, sasa polepole ndio inaelekea ukingoni na rasmi pazia litafungwa Jumapili Mei 24 kwa mechi za mwisho kuchezwa siku hiyo.
Je nani, siku hiyo Mei 24 au kabla ya hapo, atakuwa Bingwa wa msimu 2008/9?
Ni Mwenyezi Mungu tu anajua jibu lake ingawa kuna 'Watabiri' wa kila aina na wana majibu ya kila aina!!
Tunachojua, hili linasapotiwa na Wadau Wataalam, ukiaacha matokeo yasiyo tarajiwa, Arsenal ndio mwenye 'Turufu' ya nani Bingwa.
Katika mechi zake 6 alizobakisha, Arsenal atapambana na Liverpool huko Anfield tarehe 21 Aprili, Arsenal, akiwa nyumbani Emirates, atakwaana na Chelsea hapo Mei 10 na mechi moja kabla ya mechi yao ya mwisho, huko Old Trafford, Arsenal atavaana na Manchester United.
Arsene Wenger, Meneja wa Arsenal, anaamini sana wao ndio 'watamtengeneza Bingwa'.
Arsene Wenger anasema: 'Ndio sisi pengine tutaamua nani Bingwa! Lakini kwetu hilo si muhimu, muhimu ni kumkimbia Aston Villa anaetufuata na kisha kuwakaribia Chelsea na Liverpool, halafu tutajua nini kinaendelea! Lakini naamini Man U wana nafasi kubwa kutwaa Ubingwa kwani mechi yao ya mkononi [dhidi ya Portsmouth]wanachezea Old Trafford'
Wakati Arsene Wenger akitoa msimamo wake, 'vita ya msituni' iliyoaanzishwa na Rafa Benitez, Meneja wa Liverpool, huku akielekeza 'mashambulizi; yake kwa Sir Alex Ferguson, Meneja wa Man U, ilikuwa ikizidi kupamba moto.
Vita hii ilianza rasmi Januari pale Benitez alipotoa tuhuma kuwa Timu ya Ferguson inapendelewa na Ferguson akajibu kwa ufupi kwa kusema kuna kitu kinamtia hasira Benitez.
Wakati huo, Benitez alikuwa mgonjwa na alifanyiwa operesheni kadhaa kutoa vijiwe kwenye figo zake.
Wiki iliyopita, siku moja kabla Liverpool haijacheza na Chelsea kwenye Robo Fainali ya UEFA CHAMPIONS LEAGUE, Benitez akihojiwa na Waandishi wa Habari kuhusu pambano hilo ambalo hata hivyo Liverpool aliambua kipigo cha 3-1 nyumbani Anfield, aliwashangaza wengi pale alipomrukia Sir Alex Ferguson na kudai Ferguson anaiogopa Liverpool badala ya kuongelea pambano lao na Chelsea.
Baadae, Sir Alex Ferguson akihojiwa, alijibu ni jambo la kushangaza kusikia akizungumziwa yeye badala ya mechi ngumu inayoikabili timu na akaongeza: 'Ukiniuliza swali kuhusu timu nyingine, ntakupa maoni yangu! Hilo si kosa mbona Wenger wiki chache zilizopita alizungumzia Man U na akatoa jibu zuri tu bila kutukandya? Kitu cha ajabu, Rafa Benitez ana mechi ngumu na Chelsea na anahojiwa kuhusu mechi hiyo, yeye anamzungumzia Alex Ferguson! Sikujua kama mimi ni mtu muhimu sana!!'
Baada ya kujibu hivyo, hapo hapo Ferguson akaulizwa kama huwa anamkera, kumchemsha na kumuudhi Benitez kwa makusudi, Ferguson akacheka 'kifisadi' na kujibu: 'Sina jibu.'
Lakini Ferguson akaongeza: 'Nadhani Chelsea ule ushindi mkubwa kwa Liverpool umewapa morali kubwa na wao ndio watakuwa tishio kwetu na si Liverpool. Kwa sasa tumebakisha mechi 7 kwenye ligi. Muhimu ni pointi tu na kumaliza mechi moja baada ya nyingine. Hatuifikirii hiyo mechi moja mkononi.'

Mechi zilizobaki: [Timu inayotajwa kwanza iko nyumbani]:


ARSENAL

21 Aprili: Liverpool v Arsenal

26 Aprili: Arsenal v Middlesbrough

2 Mei: Portsmouth v Arsenal

10 Mei: Arsenal v Chelsea

16 Mei: Man U V Arsenal

24 Mei: Arsenal v Stoke

CHELSEA

22 Aprili: Chelsea v Everton

25 Aprili: West Ham v Chelsea

2 Mei: Chelsea v Fulham

10 Mei: Arsenal v Chelsea

17 Mei: Chelsea v Blackburn

24 Mei: Sunderland v Chelsea

LIVERPOOL

21 Aprili: Liverpool v Arsenal

25 Aprili: Hull v Liverpool

3 Mei: Liverpool v Newcastle

9 Mei: West Ham v Liverpool

17 Mei: West Brom v Liverpool

24 Mei: Liverpool v Tottenham

MAN U

22 Aprili: Man U v Portsmouth

25 Aprili: Man U v Tottenham

3 Mei: Middlesbrough v Man U

10 Mei: Man U v Man City

13 Mei: Wigan v Man U

16 Mei: Man U v Arsenal

24 Mei: Hull v Man U

No comments:

Powered By Blogger