Saturday 11 October 2008


BOSI WA HULL CITY, PHIL BROWN, NDIE MENEJA BORA SEPTEMBA!!

Phil Brown, Meneja wa Hull City, timu iliyopanda daraja msimu huu kuingia LIGI KUU, ameshinda tuzo ya kuwa MENEJA BORA LIGI KUU UINGEREZA kwa mwezi wa Septemba.
Timu ya Phil Brown, Hull City ilianza mwezi Septemba kwa kuwafunga Newcastle 2-1, wakatoka suluhu ya 2-2 na Everton, kisha wakaonyesha maajabu makubwa pale walipowafunga vigogo Arsenal kwa bao 2-1 tena Arsenal wakiwa nyumbani kwao Emirates Stadium.
Jumapili iliyopita, Hull City waliendeleza wimbi la ushindi pale waliposhinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Tottenham.
Tuzo hii ya Meneja Bora wa Mwezi hutolewa na Wadhamini wa LIGI KUU BARCLAYS.
Mshindi huteuliwa na bodi yenye wawakilishi kutoka FA, Vyombo vya Habari na Mashabiki.

NAE ASHLEY YOUNG APATA TUZO YA MCHEZAJI BORA MWEZI SEPTEMBA

Winga wa Aston Villa Ashley Young ametuzwa kuwa MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU kwa mwezi wa Septemba na hii ni mara yake ya pili kwa mwaka huu kwani msimu uliopita alipata tuzo hii mwezi Aprili.
Winga huyu mwenye miaka 23 alifunga mabao mawili na kuwatengenezea wenzake kufunga mabao mawili kwa mwezi Septemba na kuifanya Timu yake Aston Villa kushinda mechi 3 mfululizo kwa mwezi Septemba.
Ashley Young sasa ameingia orodha ya Wachezaji wachache waliomudu kushinda tuzo hii zaidi ya mara moja. Wengine walioko kwenye orodha hiyo ni Cristiano Ronaldo, Wayne Rooney na Steven Gerrard.

No comments:

Powered By Blogger