Saturday, 11 October 2008

ENGLAND WAISHINDILIA KAZAKHSTAN 5-1

Timu ya Taifa ya Uingereza ndani ya Uwanja wa kwao Wembley mjini London wamewabamiza Kazakhstan mabao 5-1 katika mechi ya Kundi la 6 la Nchi za Ulaya kuwania nafasi za kuingia FAINALI KOMBE LA DUNIA AFRIKA KUSINI 2010.
Magoli ya England yalifungwa na Nahodha Rio Ferdinand dakika ya 52 na dakika ya 64 Kazakhstan walijifunga wenyewe kufanya gemu iwe 2-0 lakini kosa kubwa la Beki Ashley Cole wa England liliwapa zawadi Kazakhstan kupata bao.
Lakini kifaru Wayne Rooney akawapatia England mabao mawili katika dakika za 76 na 86.
Jermaine Defoe akamalizia bao la 5 kwenye dakika ya 90.
Aliechaguliwa nyota wa mechi ni Wayne Rooney ingawa kwa mashabiki wengi David Beckham alieingizwa kipindi cha pili ndie alikuwa nyota wao kwani walimshangilia kupita kifani.
Kwa mechi ya leo David Beckham amefikisha mechi 106 kuchezea Timu ya Taifa ya Uingereza sawa na Sir Bobby Charlton na wote kwa pamoja sasa wanashika nafasi ya tatu kwa kuichezea England mechi nyingi.
Nafasi ya kwanza inashikwa na Kipa Peter Shilton aliechezea mechi 125 na ya pili inashikwa na Bobby Moore aliekuwa Nahodha wa England pale waliponyakua Ubingwa wa Dunia mwaka 1966 kwa kucheza mechi 108.

No comments:

Powered By Blogger