Friday 10 October 2008

CHELSEA WADAI MABILIONI MAHAKAMANI KUHUSU UHAMISHO WA MIKEL OBI

Klabu ya Chelsea imeishitaki Klabu ya FC Lyn Oslo ya Norway pamoja na aliekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Klabu hiyo Morgen Andersen kuhusu uhamisho wa Mchezaji Jon Mikel Obi wakidai warudishiwe Pauni Milioni 16 walizolipia uhamisho wake kwa sababu walidanganywa kuwa Mikel Obi alikuwa na mkataba na Klabu hiyo.
Mashtaka haya yanafuatia kupatikana na hatia kwa Mkurugenzi Mkuu huyo wa zamani wa Klabu hiyo ya Norway,Morgen Andersen, kwenye Mahakama ya Norway kwamba aligushi mikataba kuhusu Mchezaji huyo Jon Mikel Obi.
Mwezi Juni, 2006, Chelsea waliilipa Klabu ya FC Lyn Oslo Pauni Milioni 4 na Manchester United Pauni Milioni 12 kwa ajili ya uhamisho wa Mikel Obi. Wakati huo Jon Mikel Obi alikuwa tayari ameshasaini mkataba kujiunga na Manchester United ingawa baadae Obi aligoma kwenda Man U akidai mapenzi yake yako Chelsea na ndipo Man U wakalifikisha suala hilo FIFA na baadae Chelsea wakakubali kuilipa Man U.
Chelsea imetoa tamko rasmi kuhusu sakata hili kwa kusema: 'Wakati wa uhamisho wa Obi, Chelsea, Lyn na Man U tulikubaliana kulipia malipo ya Pauni Milioni 16 na kwamba huo ndio utakuwa mwisho wa sakata la Mchezaji Obi. Lakini, kwa sababu sasa Mahakama imedhihirisha kwamba kiongozi wa Klabu ya Lyn alidanganya basi sisi tunawadai wao pesa zetu!'
Chelsea ilimalizia tamko hili kwa kusema waziwazi mashtaka yao yanawahusu Klabu ya Lyn na Mkurugenzi Mkuu wao Morgan Andersen pekee na sio Manchester United.

No comments:

Powered By Blogger