Tuesday 16 December 2008

MAN U haikati rufaa kupinga adhabu ya EVRA!!!

Manchester United imeamua kutokata rufaa kupinga adhabu ya kufungiwa mechi 4 na faini ya Pauni 15,000 ya Mchezaji wao Patrice Evra aliyopewa na FA baada ya kupatikana na hatia ya kupigana na Mfanyakazi mkata nyasi wa Uwanja wa Chelsea, Stamford Bridge, aitwae Sam Bethell, ugomvi uliotokea mara baada ya mechi kati ya Chelsea na Man U msimu uliopita.
Meneja wa Man U Sir Alex Ferguson alistushwa na kukasirishwa na adhabu hiyo aliyoiita 'ni uamuzi mbovu ambao sijawahi kuuona!'.
Katika taarifa yake, Klabu ya Manchester United imesisitiza kwamba adhabu hiyo haikustahili, ina kasoro nyingi na kuikatia rufaa ni kupoteza muda hasa wakati klabu inaingia awamu ya pili ya LIGI KUU.
Vilevile, Man U wamesema kumfungia Mchezaji mechi 4 ambae hajawahi kupewa Kadi Nyekundu hata moja wakati wale wanaocheza rafu mbaya sana na wale wanaolipiza kwa kuwarushia Watazamaji vitu walivyorushiwa kufungiwa mechi 3 tu, ni ukiukwaji mkubwa wa haki.
Evra, ambae kwa sasa yuko Japan pamoja na kikosi kamili cha Man U kitakachoshiriki Mashindano ya Klabu Bingwa Duniani, atazikosa mechi za LIGI KUU za Man U watakapocheza na Stoke na Middlesbrough, Kombe la FA dhidi ya Southampton hapo tarehe 3 Januari 2009 na pambano la kwanza la Nusu Fainali ya Kombe la Carling dhidi ya Derby litakalochezwa siku nne baadae.
Mechi yake ya kwanza anayoweza kurudi uwanjani itakuwa ni pambano la kukata na shoka la LIGI KUU litakalofanyika Old Trafford dhidi ya klabu iliyomtia matatizoni, Chelsea, hapo tarehe 11 Januari 2009.

No comments:

Powered By Blogger