Thursday 22 January 2009

Man City wagundua pesa hazinunui mapenzi!!!

Klabu ya Manchester City hivi sasa, polepole, wanaanza kugundua kuwa utajiri haununui mapenzi ya dhati baada ya Klabu hiyo kuwakosa Mchezaji mmoja baada ya mwingine waliomo kwenye Listi ya Wachezaji wanaowawinda!!
Man City ilinunuliwa na Koo tajiri sana ya Kifalme kutoka Abu Dhabi ambayo ni sehemu ya nchi tajiri ya Falme za Nchi za Kiarabu inayojumuisha pia mji wa Dubai.
Ni hivi juzi tu dunia ilistushwa kuskia Staa wa Brazil Kaka anaechezea AC Milan yuko mbioni kujiunga na Man City kwa uhamisho ambao ungekuwa rekodi ya dunia wa Pauni Milioni 100 na pia angelipwa mshahara wa Pauni Laki 500 kwa wiki ambayo pia ingekuwa ni rekodi ya dunia.
Wakati kila mtu akiamini ni mwenda wazimu tu ndie atakaekataa ofa kama hiyo, Kaka aligoma kwenda Man City kwa madai anaipenda AC Milan!
Kufuatia sakata hilo habari nyingi zimeibuka kwamba si Kaka tu aliegoma kwenda Man City ingawa Klabu hiyo ilikuwa inatoa ofa za ajabu!!
Wakati mwingine Man City walikwaa kizingiti cha klabu zilizo na tamaa ya kupindukia na zilizokuwa zikidai zilipwe ada za juu mno kupita kiasi.
Wachezaji walengwa wa Man City walikuwamo Masupastaa David Villa, Kipa Gianluigi Buffon na Thierry Henry.
Mwezi Desemba, msafara kutoka Man City ulitua Valencia ukiwa na kitita cha kuwasaini David Villa na mwenzake wa hapo Klabuni Valencia David Silva.
Kitita hicho kilikuwa ni Pauni Milioni 100 kwa Wachezaji hao wawili!
Valencia wakakaza uzi na kutaka walipwe Pauni Milioni 135 kwa Wachezaji hao wawili.

Mhusika mmoja mkuu kutoka Man City alieshiriki majadiliano ya Wachezaji hao wawili ambayo hayakukamilika anasema: 'Nia yao ilikuwa tuwape mtaji wa kuendesha klabu yao kwa miaka minne!'
Baada ya hapo msafara huo uliojaa 'vijisenti' wa Man City ukatua Turin kufungua majadiliano juu ya uhamisho wa Kipa wa Italia Gianluigi Buffon anaedakia Juventus.
Juventus wakata walipwe Pauni Milioni 100 kwa kipa huyo 'anaezeeka'!!
Msafara wa Man City ukapanda ndege kurudi Manchester huku mmoja wao akilalamika: 'Sisi sio wajinga! Tumeshindwa kukamilisha uhamisho wa Wachezaji hao watatu kwa sababu klabu zao zinadhani tuna pesa za kutupa tu! Na hata Wachezaji wenyewe wamekuwa wakitaka walipwe vitu visivyowezekana! Nadhani kuna dhana potofu sisi ni matajiri mno na tuna uwezo wa kumnunua Mchezaji kwa bei yeyote!'
Ingawa majadiliano yaliyomhusu Thierry Henry yalifika hatua nzuri lakini mwishoni yalipiga chini pale Henry alipokataa kwenda Man City!!
Baadhi ya wadau wanahisi Man City inakosa mvuto na wengi wanaitazama Klabu hiyo kama Klabu duni ukilinganisha na nyingine za LIGI KUU England kama Vigogo Man U, Arsenal, Chelsea na Liverpool.
Wadau hao wanaamini bila kusita kuwa endapo 'vijisenti' hivyo vingekuwa mikononi mwa Vigogo hao, bila shaka na bila kusita, Kaka, Villa, Silva na wengine wengi walio Nyota wasingefikiria mara mbili kujiunga!
Bila shaka, mapenzi ya dhati huenda yanapatikana pasipo ndururu!!


De Jong ajiunga Man City

Mchezaji Kiungo wa Kimataifa wa Uholanzi anaechezea Hamburg ya Ujerumani, Nigel de Jong, amejiunga Manchester City kwa mkataba wa miaka minne na nusu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alikuwa na kipengele kwenye mkataba wake na Hamburg kuwa anaweza kuihama Klabu hiyo mwisho mwa msimu huu kwa Pauni Milioni 1 Laki 8 tu lakini inaaminika Man City imelipa Pauni Milioni 18 kumnunua kwa sasa ikiwa ni miezi minne tu kabla msimu haujaisha!
De Jong amechezea mechi 66 hapo Hamburg tangu ahamia akitoka Ajax mwaka 2006 uhamisho ambao uligharimu Pauni Milioni 1 Laki 2 tu.
Katika dirisha hili la uhamisho la Januari, Man City wamewanunua Wayne Bridge kutoka Chelsea na Craig Bellamy kutoka West Ham.
Man City kwa sasa wako nafasi ya 11 kwenye msimamo wa LIGI KUU England wakiwa pointi 4 toka kwenye zile timu zilizo nafasi ya kuporomoka daraja
.

No comments:

Powered By Blogger