Wednesday 21 January 2009

Man U waingia FAINALI KOMBE LA CARLING!
-Wachezaji wao Evans, Anderson na Rafael waumia!
-Mdhamini wao AIG kutoongeza tena mkataba 2010!

Mabingwa wa England, Ulaya na Dunia, Manchester United, wamefuzu kuingia Fainali ya Kombe la Carling baada ya kuifunga Derby County mabao 4-2 huko Old Trafford na hivyo kuwatoa kwa jumla ya mabao 4-3 kwani Derby walishinda mechi ya kwanza kwa bao 1-0.
Man U wakicheza na Wachezaji wengi chipukizi walifunga mabao yao kupitia kwa Nani, dakika ya 16, O'Shea [22], Tevez [34] na Ronaldo alieingizwa kipindi cha pili [penalti dakika ya 89].
Wafungaji wa Derby ni Barnes [80] na kwa penalti [90].
Leo inachezwa Nusu Fainali nyingine kati ya Burnley na Tottenham huku Tottenham wakiwa washindi wa mechi ya kwanza kwa mabao 4-1 na mshindi kati ya timu hizi atakutana na Man U Fainali hapo tarehe 1 Machi 2009.
Ushindi huo wa Man U umekuja kwa gharama kubwa kwani Wachezaji wao Johnny Evans, Anderson na Rafael waliumizwa na huenda wakakosekana kwa wiki kadhaa.
Wakati huohuo, Wadhamini wa Man U, Kampuni kubwa ya Bima AIG ambayo maandishi yake 'AIG' huonekana kifuani mwa jezi za Man U wametangaza hawataongeza mkataba wao hapo utakapoisha mwaka 2010.
AIG ni moja ya Makampuni makubwa huko Marekani yaliyokumbwa na hali mbaya ya uchumi na ilibidi Serikali ya Marekani iingilie na kuwapa mtaji ili wasifilisike.

Portsmouth wamsaini Pennant kwa mkopo

Portsmouth wamemchukua Winga wa Liverpool Jermaine Pennant kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu.
Pennant msimu huu hana namba Liverpool na ameweza kucheza mechi 4 tu tangu msimu uanze.


Robinho atimka kambini, ajitetea matatizo ya kifamilia yamemsibu!!

Mara tu baada ya kujulikana Manchester City wameshindwa kumchukua nyota wa Brazil Kaka kutoka AC Milan baada ya nyota huyo kugoma kuhamia huko, nyota mwingine wa Brazil, Robinho, ambae alikuwa kwenye kikosi cha Man City kilichokuwa kambini nchini Spain kikifanya mazoezi huko kwa sababu wikiendi hii timu hiyo haina mechi kwa vile zinachezwa mechi za Kombe la FA tu na wao wameshatolewa, mchezaji huyo alikimbia kambini na kuelekea kwao Brazil.
Robinho amejitetea hakuondoka kambini kwa hasira kwa Klabu hiyo kumkosa Kaka bali ni kwa sababu ya matatizo ya kifamilia.
Robinho anaetimiza miaka 25 hapo Januari 25 inasadikiwa alikwaruzana na Meneja Mark Hughes kabla ya kutimka.

Palacios atua Tottenham!

Kiungo kutoka Honduras, Wilson Palacios anaechezea Wigan, amenunuliwa na Tottenham kwa dau la Pauni Milioni 12.
Palacios alijiunga na Wigan Januari 2008 kwa dau kiduchu la Pauni Milioni 1 tu!

Middlesbrough matatani na FA!!
Mameneja wa Newcastle na Hull City pia kizimbani FA!!

Klabu ya Middlesbrough inatakiwa ijibu mashtaka na FA, Chama cha Soka England, kwa kosa la utovu wa nidhamu wa Wachezaji wake waliouonyesha kwa Refa Mark Hasey walipocheza na West Bromwich na kufungwa 3-0 mara tu baada ya mwenzao Didier Digard kulambwa Kadi Nyekundu kwa rafu mbaya dhidi ya Borja Valero.
Wachezaji kadhaa wa Middlesbrough walimzonga Refa huyo na kusababisha adondoshe moja ya Kadi zake.
Middlesbrough wamepewa mpaka tarehe 4 Februari 2009 kuwasilisha utetezi.
Wakati huohuo, Mameneja wa Newcastle Joe Kinnear na Phil Brown wa Hull City pia wameshtakiwa na FA kwa utovu wa nidhamu baada ya wao kukwaruzana pembeni mwa uwanja huku timu zao zikicheza mechi ya marudiano ya kuwania Kombe la FA hapo Januari 14 na ikabidi Refa Phil Dowd aingiilie na kuwatoa nje ya uwanja wote wawili.
Msuguano wao ulitokea pale Fabio Coloccini wa Newcastle alipomchezea rafu Daniel Cousin wa Hull.
Hii ni mara ya 3 kwa Joe Kinnear kushtakiwa na FA tangu achukue madaraka Septemba 2008 hapo Newcastle.
Kinnear na Brown wamepewa hadi Februari 3, 2009 kuwasilisha utetezi.

No comments:

Powered By Blogger