Tottenham chupuchupu kuikosa Fainali Carling Cup, wafungwa ila wamo!!!
Klabu ya Tottenham iliyo LIGI KUU England jana ilifungwa na Timu ya Darala la chini, Burnley, kwa mabao 3-2 lakini ilisonga mbele na kuingia Fainali ya Kombe la Carling kwa vile walishinda mechi ya kwanza waliyochezea kwao White Hart Lane kwa mabao 4-1.
Na laiti ingekuwa ile sheria ya mabao ya ugenini kuhesabiwa mawili endapo timu zinakuwa sawa kwa mabao mwisho wa mchezo basi Tottenham angekuwa marehemu kwani hadi mwisho wa gemu hiyo Burnley alikuwa kashinda 3-0 na hivyo kufanya jumla ya magoli kuwa 4-4 kwa mechi mbili.
Bahati mbaya kwa Burnley na nzuri kwa Tottenham ni kwamba sheria hiyo kwenye Kombe hili inatumika baada ya dakika 120!
Hivyo mpaka dakika 90 kwisha, ingawa Burnley alikuwa mbele 3-0 mechi iliongezwa nusu saa ya nyongeza na laiti matokeo yangekuwa hayo hayo 3-0 hadi mwisho Burnley angeingia Fainali.
Lakini katika hiyo nusu saa ya nyongeza Tottenham walipachika mabao 2 na kufanya mechi kuisha Burnley mshindi 3-2 lakini imetolewa kwa jumla ya magoli 6-4!
Sasa, Tottenham ambae ndie Bingwa mtetezi wa Kombe la Carling atapambana Fainali na Manchester United hapo tarehe 1 Machi 2009.
Abramovich alishitaki gazeti la Sunday Times!!!
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich, amelishitaki gazeti la Uingereza Sunday Times na kudai fidia baada ya gazeti hilo kuandika kwamba tajiri huyo anataka kuiuza klabu yake hiyo.
Katika makala yake ya uchumi, gazeti hilo lilidai Abramovich yumo mbioni kuiuza klabu hiyo kwa Waarabu wa Ghuba au Koo ya Kifalme ya Saudi Arabia.
Mbali ya kudai fidia, Abramovich anataka mahakama ilizuie gazeti hilo kurudia madai hayo.
Wachezaji wa Newcastle watwangana makonde mazoezini!!!
Meneja wa Newcastle Joe Kinnear amesema hatochukua hatua zozote dhidi ya Wachezaji Charles N'Zogbia na Andy Carrol waliochapana makonde mazoezini juzi siku ya Jumanne.
Wachezaji hao walionyesheana ubabe na ilibidi waamuliwe mara kadhaa baada ya kuchezeana rafu mazoezini.
Ugomvi huo umekuja muda usiozidi wiki tangu Newcastle abamizwe 3-0 na Blackburn na kwenye mechi hiyo Watazamaji waliwashuhudia Wachezaji wa Newcastle Joey Barton na Jose Enrique wakibatukiana kwa hasira uwanjani huku mechi ikiendelea.
Newcastle ipo kwenye hali tata na hata Meneja mwenyewe Joe Kinnear ana kesi 3 za kujibu kwenye Kamati ya FA baada ya kushitakiwa kwa kukosa nidhamu kuhusiana na matukio mbalimbali yanayomhusu kwenye mechi za Newcastle.
Mpaka sasa Newcastle inasuasua nafasi ya 14 kwenye msimamo wa LIGI KUU England wakiwa pointi 2 tu juu ya timu zilizo kwenye ile n'ngwe hatari ya kushushwa daraja.
No comments:
Post a Comment