Thursday, 22 January 2009

UHONDO WA LIGI KUU England: Msimu huu hautabiriki!!!

Wakati duru ya kwanza ya Ligi hii yenye jumla ya Timu 20 imeshamalizika, hakuna hata shabiki mmoja anaeweza kubashiri nani ataibuka Bingwa na Timu zipi 3 zitaporomoka daraja!
Mpaka sasa kitu kilichoibuka na kuwa dhahiri kabisa ni kuonekana kwa matabaka matatu katika msimamo wa Ligi hii.
Tabaka la kwanza ni lile linalojumuisha Klabu Vigogo kama Manchester United, Liverpool, Chelsea na Arsenal huku Aston Villa na pengine Everton wakivamia kundi hilo.
Tabaka hili ni lile la timu zinazoongoza msimamo wa Ligi na kuziacha nyingine zote kwa mbali kidogo.
Mpaka sasa, Man U, ingawa amecheza mechi moja pungufu, anaongoza akiwa na pointi 47 wakiwa sawa na Liverpool alie nyuma kwa sababu ya idadi ndogo ya tofauti ya magoli.
Nafasi ya 3 ni Chelsea wakiwa na pointi 45, wa nne ni Aston Villa pointi 44, wa tano Arsenal pointi 41 na wa sita kwenye kundi hili ni Everton akiwa na pointi 36.
Tabaka la pili lina Timu tatu ambazo ndio hasa zinastahili kuwa hapa na nazo ni Wigan [pointi 31], West Ham [29] na Hull City [27].
Zingine ambazo pengine unaweza kuziingiza hapa ni Fulham, ambao wamecheza mechi 2 pungufu, wakiwa na pointi 26 na hata Man City [pointi 25].
Tabaka la tatu ni zile timu zinazopigania kuzikimbia nafasi za 18, 19 na ya 20 kwenye msimamo wa Ligi kwa sababu hiyo ni 'Denja Zoni', yaani, Timu inayoshika nafasi yeyote kati ya hizo tatu mwisho wa ligi basi inashushwa daraja.
Utamu mkubwa wa Ligi ya msimu huu, mbali ya kutokuwa na fununu hata chembe wa nani anaunusa Ubingwa, upo kwenye tabaka hili lenye Timu 9 zinazogombea kuzikimbia nafasi ya 18, 19 na 20!!
Cha ajabu mno, kati ya Timu hizo 9, ya juu kabisa mpaka sasa iko nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi na iko pointi 3 tu juu ya Timu ambazo kwa sasa zinashikilia nafasi hizo za 'denja' za 18, 19 na 20!
Kingine cha kustaajabisha ni kuwa kwa sasa timu zote 3 zilizo kwenye 'Denja Zoni', yaani Middlesbrough alie nafasi ya 18, Stoke City nafasi ya 19 na wa mwisho kabisa ni West Bromwich Albion kwenye nafasi ya 20, wana pointi sawa kabisa, wote wakiwa na pointi 21 na wametofautishwa tu kwa tofauti ya magoli!!
Timu nyingine zenye pointi 21 pia na wako juu tu ya Timu hizo zilizo mkiani kwa idadi ya magoli tu ni Timu iliyo nafasi ya 17 Blackburn Rovers na Tottenham walio nafasi ya 16.
Juu ya Tottenham zipo Timu 3 nyingine zenye pointi 23 kila moja na hizo ni Sunderland [nafasi ya 15], Newcastle [14] na Bolton [13].
Kwenye nafasi ya 12 yuko Portsmouth mwenye pointi 24.
Hayo ndio maajabu ya LIGI KUU England msimu huu na ni dhahiri hili ndilo linaloifanya Ligi hii kuwa na ushindani, uhondo na kutokutabirika vitu vyote ambavyo vinailetea sifa ya kuwa LIGI BORA DUNIANI tofauti na Ligi nyingi zenye Maskandali ya rushwa na upangaji matokeo!!

No comments:

Powered By Blogger