Tuesday, 2 March 2010

Umiliki Man United: Vizito ‘Wakombozi Wekundu” wakutana kuiteka toka kwa kina Glazer!!!
Matajiri wakubwa ambao ni Masapota wakubwa wa Manchester United waliovumishwa kutaka kuinunua Klabu ya Manchester United kutoka kwa Familia ya Kimarekani ya kina Glazer wamekutana kwa mara ya kwanza kujadili mbinu na mikakati ya kuing’oa Klabu hiyo kutoka mikononi mwa Wamarekani hao walioingiza Man United kwenye deni la zaidi ya Pauni Milioni 700.
Kundi hilo, lilobatizwa jina la “Wakombozi Wekundu” limeunga mkono harakati za Masapota wa Klabu wanaojiita ‘MUST’ ‘[Manchester United Supporters Trust] wanaoendesha upinzani kwa ishara ya rangi za Kijani na Dhahabu, ambazo zilikuwa ni jezi za Klabu anzilishi ya Man United, Newton Heath, na pia limesema wao wanawapinga kina Glazer tu na wanaridhishwa na kazi na utawala wa Mkurugenzi Mtendaji David Gill pamoja na Meneja Sir Alex Ferguson.
‘Wakombozi Wekundu” hao ni kundi linalowaunganisha Matajiri Wakubwa ambao ni Wapenzi wa damu wa Manchester United kina Jim O’Neill, ambae ni Mchumi, Mwanasheria Mark Rawlinson na Mtaalam wa Fedha Keith Harris.
Habari toka ndani ya Kundi hilo lilithibitisha kuwepo Mkutano wao na pia kusema sasa wanafanyia kazi mbinu za kuiteka Man United na wamewataka Mashabiki wote wa Manchester United duniani kote kuwasaidia.
Hata hivyo, Msemaji wa Familia ya Glazer amesema Klabu haiuzwi.
FIFA: Bondeni wako tayari kwa Kombe la Dunia!
Mkuu wa FIFA Sepp Blatter amesema Afrika Kusini iko tayari kabisa kwa Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Nchini humo kuanzia Juni 11.
Kumekuwa na minong’ono ya muda mrefu kuwa hali si nzuri katika matayarisho ya Fainali hizo lakini Blatter ameondoa shaka hiyo huku ikianza hesabu ya siku 100 kabla ya Fainali hizo.
FIFA imetamka mpaka sasa zimeshauzwa Tiketi Milioni 2.2 kati ya jumla ya Tiketi Milioni 2.9 ingawa uuzwaji unaendelea polepole mno.
Inategemwa Wageni zaidi ya 450,000 watatua Afrika Kusini katika Fainali hizo.
Blatter alitoa kauli yake mara baada ya kutembelea Viwanja 10 vitakavyochezwa mechi za Fainali na kushuhudia vyote vikiwa vimekamilika.

No comments:

Powered By Blogger